Wananchi mtaa wa Kigala uliopo kata ya Buswelu ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kukubaliana kwa masuala yote yenye manufaa kwa jamii huku akiwaasa wananchi hao kukubali kutoa eneo kuruhusu ujenzi wa zahanati kuanza wakati masuala ya fidia yakiendelea kushughulikiwa.
Rai hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe.Dkt.Angeline Mabula wakati wa muendelezo wa ziara zake za kusikiliza kero na kukagua miradi ya maendeleo kata kwa kata wakati wa mkutano wa hadhara katika mtaa wa Kigala.
Akijibu kero ya Mgeni Juma mkazi wa mtaa wa Kigala Mhandisi Uswege Jacob kutoka wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) amesema TARURA inaendelea kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kurekebisha miundo mbinu ya barabara huku akikiri uwepo wa mtandao mkubwa wa barabara wa zaidi ya 1900km huku bajeti ikilenga mtandao wa 800km.
"..tunayo changamoto ya ufinyu wa bajeti kukidhi matengenezo ya barabara zote kwa mara moja.Tunachofanya ni marekebisho madogomadogo kuwezesha barabara hizo kupitika na punde fedha zitakapopatikana zitajengwa.."
Kuhusu kero za Ardhi Grace Massawe Afisa Ardhi wa Manispaa ya Ilemela amesema hati sio mwisho wa haki kama itagundulika kuna watu waliopata hati miliki bila kufuata utaratibu mchakato wa kufuta hati hizo utafanyika mara moja ili kurudisha viwanja kwa wamiliki halali.
Nae mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Jeremiah Lugembe amesema suala la ulipaji wa fidia linaendelea kadri ya fedha za makusanyo ya ndani zinavyopatikana huku akiwahakikishia wananchi wa kata ya Buswelu ukuta wa shule ya msingi Kaserya kujengwa na mradi wa uboreshaji miundo mbinu ya miji na mazingira (TACTIC) wanaojenga barabara ya Buswelu - Busenga- Coca cola 3.3km unaofadhiliwa na benki ya dunia.
Mhe.Mabula amewataka wananchi hao kuungana ili kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati unaosuasua kwa sasa kutokana na wenyeji wa maeneo hayo kudai kulipwa fidia kwanza.
Akihitimisha mkutano huo Mhe.Mabula amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kuanzia tarehe 11- 20 Oktoba 2024 kwa ajili ya kupiga kura na watakaoweza kugombea kuomba nafasi mbalimbali.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.