Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuiunga mkono timu ya mpira wa miguu ya Pamba Jiji ili iweze kufanya vizuri katika mashindano ya ligi kuu ya Tanzania bara.
Hayo yamesemwa na mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Ilemela ambae pia ni Katibu tawala wa wilaya hiyo Wakili Adv. Mariam Abubakar Msengi wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa tawi la timu hiyo katika viwanja vya stendi ya daladala Pasiansi ambapo akawataka kuhakikisha wanajitoa kwa hali na mali kuunga mkono harakati zote zitakazochangia timu hiyo kufanya vizuri .
'.. Uzinduzi wa tawi hili uende sambamba na uungwaji mkono kwa timu yetu, hii ndio timu ya wana Ilemela, hii ndio timu ya kanda ya ziwa, hii ndio timu yetu watu wa Mwanza ..' Alisema
Aidha Wakili Msengi akamshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan kwa juhudi zake za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na mpango wake wa ukarabati wa uwanja wa mpira wa miguu wa CCM Kirumba kwa ajili ya matumizi ya mashindano ya AFCON na ujenzi wa kituo kipya cha michezo kata ya Buswelu .
Kwa upande wake afisa michezo Jiji la Mwanza ambae pia ni mjumbe wa Kamati ya uhamasishaji Ndugu Mohamed Bitegeko akafafanua kuwa timu ya Pamba Jiji inaendesha kampeni ya kuhamasisha wananchi kununua jezi kwa thamani ya shilingi elfu thelathini na ununuzi wa tiketi kwa madaraja tofauti tofauti ili kuisaidia timu hiyo kiuchumi na kuleta hamasa kwa wananchi ili kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali .
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi. Ummy Mohamed Wayayu akaongeza kuwa manispaa yake itaendelea kushirikiana na uongozi wa timu hiyo ili kuisaidia kufikia malengo yake pamoja na kuahidi kununua tiketi kwa ajili ya madiwani na watumishi wa manispaa ili waweze kushiriki sherehe za siku ya timu ya mpira wa miguu ya Pamba Agosti 10, mwaka huu
Uzinduzi wa tawi hilo ulienda sambamba na ukaguzi wa kikosi cha timu ya mpira wa miguu ya walimu wanaume itakayoshiriki mashindano ya shirikisho la michezo la watumishi wa Serikali za mitaa (SHIMISEMITA) .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.