Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia kamati yake ya Huduma,afya na elimu imefanya ziara maalum kwa kutoa elimu juu ya ugonjwa wa Korona unaosababishwa na virus vya Covid-19 kwa kupita maeneo ya masoko na stendi.
Wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa kamati Mhe.Sarah Ng’hwani ambaye pia ni Diwani wa kata ya Buswelu ameongoza timu hiyo inayoundwa na waheshimiwa madiwani na wataalam mbalimbali wa Manispaa kwa ajenda moja kubwa ya kupambana na Korona.
Akizungumza katika soko la Buswelu Mhe.Sarah amewataka wananchi wa Ilemela kuwa makini kusikiliza na kufuata maelekezo ya wataalam wa afya juu ya namna ya kuepuka na kujilinda na Korona.Sambamba na hayo Mhe.Ng’hwani amewataka wananchi wanaofanyia shughuli zao maeneo ya msongamano kama masokoni na stendi kukaa angalau mita moja kutoka kwa mtu hadi mtu kama njia mojawapo ya kupunguza uwezekano wa maambukizi kusambaa kwa kasi.
“Ugonjwa huu ni kweli sio mzaha ,wananchi tuchukue tahadhari, kuvaa barakoa sasa ni lazima”amesema.
Kamati hii pia ilifika katika soko la samaki la kimataifa Kirumba maarufu kama Mwaloni na kuongea na wananchi waliokuwepo sokoni.
“Soko hili ni la kimataifa tunapokea wageni kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi hivyo ni lazima kuchukua hatua thabiti katika kujilinda na korona tulikuwa tunaisikia nchi za nje lakini sasa hivi tunayo nchini mwetu sio masihara jamani tunawe mikono mara kwa mara kadri tuwezavyo.
Tukishindwa kufata maelekezo ya kitaalam hapa tutakufa wote na soko hili litafungwa hatutakuwa na shughuli za kutuingizia kipato. Embu tujifikirie maisha yatakuwaje” Amesema Muhasibu wa mapato wa Halmashauri ndugu Andrew Ndaba.
Ziara ya kamati hiyo iliungwa mkono na Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Ilemela kwa kugawa sabuni za maji za kunawia mikono zaidi ya lita 200 katika maeneo ya mikusanyiko ambapo kamati imepita kutoa elimu. Soko la samaki Kirumba wamepewa lita 50,soko la matunda Kirumba lita 50, Soko la Buzuruga lita 50,stendi ya mabasi Buzuruga lita 50 na soko la Nyakato lita 25.
Akizungumza wakati wa kukabidhi sabuni hizo Katibu muenezi wa UVCCM wilaya ya Ilemela Denis Kengela Kankono amesema kama vijana wa CCM wameguswa na janga hili lakini pia kitendo hicho ni katika jitihada za kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli katika mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Korona unaotesa taifa na ulimwengu mzima kwa sasa.
“Katika masuala muhimu ya kijamii kama haya tunaweka itikadi zetu zote pembeni,itikadi za kisiasa ,kidini ,ukabila nk hazina nafasi kwetu.Tunawajali na kuwapenda wananchi wetu ndo maana tunajali usalama wenu kwanza.Tunaomba wadau wengine mbalimbali wajitokeze kwa wingi katika kupambana na ugonjwa huu wa Korona.
Akitoa shukrani kwa kamati na UVCCM Mwenyekiti wa umoja wa wakala wa mabasi wa stendi ya Buzuruga ndugu Jacob Nyamatare amesema “Tunashukuru kwa kujali kwenu na kuja kutoa elimu na kutupa sabuni hizi katika kupambana na janga la Korona ila tunazidi kuwaalika tena na tena kwa ajili ya elimu isiyokuwa na mwisho kwani hapa stendi watu ni wabishi mno na hata hivyo tunapokea wageni na watu wapya kila siku”.
Aidha mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Ilemela Bi.Pili Kassimu ameeleza kwa kina dalili za ugonjwa wa Korona ambazo ni homa,kikohozi,kubanwa mbavu na kupumua kwa shida,vidonda kooni,kuumwa kichwa na mwili kuchoka.
“Mnapoona dalili hata moja wahi kituo cha afya kupata huduma.Mkumbuke tunaweza kujikinga na Korona kwa kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa,kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono,kuepuka misongamano,kusafisha mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni.Vipo vingi vya kufahamu tusikilize vyombo vya habari pia na kupenda kusoma mabango maeneo yetu ya kazi.”amesema Bi.Pili.
Akihitimisha ziara hiyo katika eneo la soko la Nyakato Mhe.Ng’hwani amewataka watendaji wa kata na viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani Ilemela kuwachukulia hatua wazazi wanaoruhusu watoto wao kuzurura hovyo mitaani kwa kuwatoza faini na kuwaripoti katika ngazi zingine za juu pindi wanapokaidi amri na utaratibu uliowekwa na serikali.
Watoto kufunga shule ni moja ya njia ya kuwakinga na kuwaepusha na maambukizi, lengo la serikali kufunga shule ni pamoja na kutetea uhai wa watoto hawa kwa kuwaepusha na msongamano ambayo ndio njia rahisi ya maambukizi kusambaa kwa haraka.Tunataka watoto wabaki nyumbani ”alihitimisha
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.