Wananchi wa wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wameshauriwa kutumia fursa ya uwepo wa madaktari bingwa wanaotoa huduma za matibabu na ushauri wa kibingwa dhidi ya magonjwa mbalimbali kwa kujitokeza na kupatiwa matibabu ya magonjwa yanayowakabili.
Rai hiyo imetolewa na mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Ilemela Dkt. Mateso Mayunga wakati wa zoezi la utoaji wa huduma kwa wananchi waliojitokeza kupata matibabu na ushauri wa kitaalam kutoka kwa madktari hao.
Dkt. Mateso ameongeza kuwa amepokea jumla ya madktari watano wanaofanya kazi chini ya kampeni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hasan kufikisha madktari bingwa katika hospitali za wilaya kusaidia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kufika katika hospitali kubwa kwa ajili ya kukutana na madaktari bingwa kupata huduma za kiafya.
'.. Tumepokea madaktari bingwa watano katika hospitali yetu ya wilaya na kiukweli tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwani si jambo jepesi kwa mwananchi wa kawaida kuwafikia madktari hawa kutokana na gharama lakini akaona awalete huku walipo waweze kupata huduma..'
Aidha amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwani halmashauri imetoa usafiri bure kuwafikisha wananchi hospitali ya wilaya na kurudi ambapo kituo ni kuanzia makao makuu ya Manispaa Buswelu .
Madaktari bingwa waliopo ni bingwa wa watoto, upasuaji, mambo ya ndani,magonjwa ya wanawake na dawa za usingizi na ganzi.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka hospitali ya chuo kikuu cha Dodoma chini ya kampeni ya Rais Dkt Samia Bi. Rehema Tagarile amefafanua kuwa muitikio wa wananchi katika kupata huduma ni mzuri na wakuridhisha huku wagonjwa wengi waliojitokeza kwake ni wale wanaosumbuliwa na magonjwa ya mfumo wa hewa na mfumo wa damu na kwamba ameweza kuwapatia matibabu, ushauri na rufaa kwa wenye uhitaji wa muendelezo wa matibabu .
Ederick Mathias Rutashobya ni mwananchi wa kata ya Bugogwa wilaya ya Ilemela ambapo mbali na kuishukuru Serikali kwa madaktari bingwa hao akaomba utaratibu huo uwe endelevu Kwa kuwa si wananchi wote wenye uwezo wa kugharamia matibabu pamoja na kuwaasa wananchi wengine kujitokeza na kutumia fursa hiyo.
Madktari hao watakwepo wilaya ya Ilemela kwa muda wa siku tano kuanzia jana siku ya jumatatu Juni 17 hadi Ijumaa Juni 21 wakihudumia wananchi kwa malipo taslimu au kugharamiwa na mfuko wa bima ya afya.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.