Wananchi wa Ilemela wamepongezwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa namna wanavyochangia na kuchochea utekelezaji wa shughuli za maendeleo ndani ya kata zao.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya Mbunge wa jimbo hilo iliyolenga kusikiliza kero, changamoto pamoja na kupokea ushauri kutoka kwa wananchi wa kata za Nyakato, Nyamhongolo na Buswelu ambapo amewapongeza wananchi hao kwa kuchangia nguvu kazi pamoja na fedha kwa ajili kutatua kero mbalimbali ikiwemo masuala ya upatikanaji wa maji pamoja na ujenzi wa shule katika kata zao.
'.. Niwapongeze kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika, kwani pamoja na fedha za Serikali, bado wananchi mnaunga juhudi za serikali kwa kuchangia nguvu zenu ..' Alisema
Sambamba na hilo Dkt Mabula amechangia kiasi cha shilingi milioni 4 kutoka mfuko wa jimbo kwa ajili ya utatuzi wa kero ya upatikanaji wa maji , shilingi laki 4 kwa ajili ya uwekaji wa umeme katika shule ya msingi Kangaye na mifuko 100 ya saruji ikiwa ni mchango wa ujenzi wa kituo cha polisi Nyamhongolo sambamba na kuwataka kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo
Mhandisi Modest Apolinary, mkurugenzi wa Ilemela akizungumzia kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na hlmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ukemavu, amesema kuwa takriban shilingi milioni 490 zimetolewa huku akiwataka wananchi wote wenye changamoto za upimaji wa ardhi kuandika malalamiko yao katika ofisi za watendaji wa kata zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Aidha mhandisi Modest amefafanua kuhusu hatua zilizofikiwa kuhusu ujenzi wa barabara kutokea Buswelu mbogamboga kupitia Nyamadoke hadi Nyamhongolo na ile ya Buswelu-Busenga hadi Cocacola na kusema kuwa hadi sasa hatua iliyopo ni ya manunuzi ambapo tayari tangazo la zabuni ya ujenzi wa barabara imeshatangazwa.
Fute David ni Mhandisi wa idara ya maji safi na maji taka ya jijini Mwanza MWAUWASA akifafanua kuhusu suala la ukosefu wa maji amewataka wananchi wa Mtaa wa Kangaye kuwa wavumilivu kutokana na kero ya ukosefu wa maji safi na salama na kwamba mamlaka yake inaendelea na juhudi za kumaliza kero hiyo kwa kujenga chanzo kipya cha maji cha Butimba, kufanya mgao wa huduma za maji ili angalau kila mwananchi apate pamoja na kuchimba visima vitakavyorahisisha upatikanaji wa huduma hiyo
Katika ziara hiyo wananchi walipata fursa ya kuwasilisha changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa huduma za maji safi na salama, ubovu wa barabara pamoja na kukatika kwa nishati ya umeme uunganishiwaji wa umeme changamoto ya zoezi la urasimishaji, kero ambazo Serikali imeahidi kuzitatua.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.