Wananchi wa Jimbo la Ilemela wametakiwa kutumia fursa ya uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura kwa ajili ya kuhakiki taarifa zao ambapo zoezi hili litaenda sambamba na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili litakaloanza tarehe 01 Mei hadi 07 Mei 2025.
Afisa Mwandikishaji wa jimbo la Ilemela Bi Ummy Wayayu alitoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili yaliyoendeshwa na tume huru ya taifa ya uchaguzi siku ya tarehe 29 Aprili 2025 kwa waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki
“Nitoe rai kwa wananchi wote wa Ilemela kuhakikisha wanatumia fursa hii kwa kupita kwenye vituo vilivyoainishwa katika kata zao ili waweze kulikagua daftari hilo, kufanya marekebisho ya taarifa zao, kuingiza au kufuta majina ya wapiga kura pamoja na kuweka pingamizi kwa mpiga kura aliyeandikishwa na hana sifa za kuwemo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili kuweza kushiriki uchaguzi mkuu”. Alisema Bi Ummy
Mafunzo hayo yalitanguliwa na uapisho kwa washiriki wa mafunzo hayo kwa ajili ya kujitoa kwenye vyama vya siasa na utunzaji wa siri ambapo yalienda sambamba na mafunzo kwa vitendo ya mfumo wa uandikishaji na vifaa vya BVR pamoja na ujazaji wa fomu lengo likiwa ni kuwajengea umahiri wa kutekeleza zoezi hilo na kuhakikisha zoezi la uboreshaji linakamilika kwa ufanisi.
Bi Ummy aliwahimiza ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wa zoezi hili na kuwasisitiza wanazingatia muda wa kufungua vituo ambao ni saa mbili kamili asubuhi kwani asingependa kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi pamoja na kuwasikiliza na kuwapa ushauri yanayopaswa kufanyika bila kutumia nguvu.
“Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili ni maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi wa kumi 2025, na hii ni kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ambapo inaitaka tume huru ya taifa kufanya uboreshaji mara mbili kati ya uchaguzi uliomalizika na kabla ya siku ya uteuzi”, alibainisha afisa uchaguzi wa Ilemela Ndugu Shilinde Malyagili.
Mohammed Maarufu afisa mwandikishaji msaidizi ngazi ya kata aliyekuwa mwenyekiti wa mafunzo hayo alimhakikishia Afisa Mwandikishaji Jimbo kuwa wamezingatia na kuyaelewa yote waliyoelekezwa na kufundishwa na kuyachukua na kuwa wako tayari kutekeleza kazi hiyo maalum.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.