Wananchi wa Ilemela wameaswa kutunza mazingira yao kwa kupanda miti mingi bila kuchoka kwa kuzingatia faida zake na ikiwa ni moja ya njia ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi sambamba na kufanya mazingira kuwa ya kuvutia zaidi.
Hayo yamezungumzwa na Afisa misitu wa Manispaa ya Ilemela Ndalahwa Bucheye wakati akitoa elimu juu ya namna bora ya kupanda miti na faida kwa wananafunzi na baadhi ya wananchi waliojitokeza kuadhimisha kumbukizi ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar inayoadhimishwa nchini kila tarehe 26 Aprili ya mwaka tangu Muungano huo ulipofanyika mnamo mwaka 1964 kupitia zoezi la upandaji miti lililofanyika katika shule mpya ya sekondari Igogwe iliyopo kata ya Bugogwa .
"Miti pia ni chanzo cha kukuza uchumi kutegemea na aina ya mti uliopanda,kama ni ya mbao utavuna na kuuza mbao na kama ni ya matunda yatauzwa na kutumika kama chakula nyumbani ,tunapopanda tuzingatie upandaji wa kitaalam ili kupata matokeo chanya ..." amesema Bucheye
Nae Alex Julius ambaye ni Mhifadhi wa misitu kutoka mamlaka ya misitu Tanzania (TFS) Ilemela amesema ni muhimu kwa wananchi kuelewa faida za miti kwa maisha ya binadamu na hapo ndipo wataona umuhimu wa kuitunza.
"Tunatumia siku hii maalum kufikisha ujumbe kwa jamii na kuihamasisha katika suala zima la upandaji miti,utunzaji na usimamizi wake ili tuwe na matumizi endelevu ya rasilimali zetu za misitu..."amesema Alex
Jumla ya miti 300 iliyotolewa na TFS ya aina mbalimbali ya mbao,vivuli na matunda kama michungwa,mapera na miparachichi imepandwa shuleni hapo huku msisitizo ukitolewa juu ya utunzwaji wake.
Helena Samwel ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule hiyo yeye anashukuru uongozi wa Manispaa kwa kuchagua kupanda miti Igogwe sekondari na kuahidi kuwa yeye na wenzake kuwa mabalozi wazuri kwa jamii juu ya masuala ya utunzaji wa mazingira na upandaji miti.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.