Jumla ya wananchi 780 wa Ilemela wamenufaika na huduma mbalimbali za kliniki ya maendeleo ya jamii ambazo zimejumuisha huduma ya mikopo ya vikundi ya asilimia 10,mikopo ya wajasiriamali fedha kutoka serikali kuu,bima ya afya iliyoboreshwa (iCHF), msaada wa kisheria,vitambulisho vya wajasiriamali, mazingira sambamba na huduma mtambuka zinazogusa jamii moja kwa moja.
Akizungumza wakati akifungua zoezi la utolewaji wa huduma hizo katika viwanja vya Furahisha vilivyopo kata ya Kirumba mwakilishi wa Mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii Yusuph Okoko amesema halmashauri imeona uhitaji mkubwa wa wananchi kufikiwa na huduma hizo jirani na maeneo yao kwa kutambua umuhimu wa kujenga uelewa wa pamoja ndani ya jamii.
" Manispaa ya Ilemela tayari imetenga shilingi milioni 920 kwa ajili ya vikundi 60 awamu ya pili inayotarajiwa kutolewa Juni 2025,ni muhimu wananchi wote kuelewa kwa undani kabla ya kufanya maamuzi ya kukopa."
Fidelis Kiraiyo ni mratibu wa ushirikishwaji jamii na bima ya iCHF amewaasa wananchi hao kujiunga na huduma hiyo ambayo inagharimu shilingi elfu 30 tu kwa kaya yenye watu kuanzia 1 hadi 6 kwa mwaka mmoja.
Nae Paskazia Muyanja ambaye ni Afisa maendeleo ya jamii kata ya Sangabuye amewataka wanawake kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuchangamkia fursa za mikopo ya 10% isiyokuwa na riba kwa kuwekeza katika miradi inayotekeleka ili kufanya zoezi la ukopeshaji kuwa endelevu.
Baraka Liwa ni mkazi wa kata ya Kitangiri amepongeza uongozi wa Ilemela kwa kubuni kliniki hiyo ambayo anasema imemfanya kuwa bora katika masuala ya matumizi ya fedha .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipanga kuhudumia wananchi 500 ambapo hadi zoezi hilo la siku moja linafungwa wananchi 780 wamehudumiwa sawa na asilimia 156 ya lengo.
|
|
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.