Wanamichezo ambao ni wanafunzi kutoka shule za sekondari Ilemela waliochaguliwa kuunda timu ya UMISETTA ngazi ya wilaya wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na nidhamu pamoja na kusikiliza maelekezo ya viongozi wao watakapokuwa katika kambi ili timu hiyo iweze kurudi na ushindi wa ngazi ya mkoa.
Rai hiyo imetolewa na afisa elimu sekondari wa Manispaa ya Ilemela Mwalimu Sylvester Mrimi wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA) yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya wavulana Bwiru sekondari yakikutanisha timu kutoka kanda nne za Buswelu, Pasiansi, Bugogwa na Bwiru.
Pamoja na hayo wanamichezo hao wametakiwa kuhakikisha wanakuwa sehemu ya wananchi watakaoshiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi ili kuisaidia Serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya mipango ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi wengine kuhesabiwa.
“Mwezi Agosti 23 tutakuwa na tukio la Sensa ya watu na makazi, Mimi nitahesabiwa, Nashauri na wana michezo washiriki kuhesabiwa ili Serikali yetu iweze kupanga mipango ya maendeleo yake”. Alisema
Kwa upande wake Mwalimu Kizito Bahati akizungumza kwa niaba ya afisa michezo wa Manispaa ya Ilemela ametoa ombi kwa vilabu vya michezo na shule za michezo vinavyopatikana mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla kusajili wachezaji wanaoibuliwa katika mashindano mbalimbali yanayofanyika ndani ya wilaya
Bi Rosemary Mkama, meneja wa benki ya NMB tawi la Ilemela amesema kuwa benki yake itaendelea kushirikiana na Serikali haswa wilaya ya Ilemela katika kufanikisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo michezo huku akiwaalika wanamichezo hao kujitokeza na kunufaika na huduma zinazotolewa na benki hiyo.
Nae mwanafunzi Salome John kutoka shule ya Sekondari Bugogwa mbali na kushukuru kwa timu yake kuibuka kuwa mshindi wa jumla ameongeza kuwa mafanikio waliyoyapata yametokana na timu yao kuwa na maandalizi ya kukutosha, kushirikiana, kusikiliza maelekezo ya mwalimu na kujituma huku akiahidi kufanya vizuri zaidi katika ngazi ya mkoa na kurudi na ushindi.
Mashindano hayo ya UMISETA yamehusisha michezo ya mpira wa miguu, mpira wa mikono, riadha, mpira wa pete, mpira wa wavu na kipekee kwa mwaka huu kumekuwepo na kipengele cha mziki wa singeli ambapo timu ya kanda ya Bugogwa imeibuka mshindi wa kipengele hicho kipya cha singeli pamoja na kutwaa ubingwa wa jumla kuwa mshindi wa kwanza na kutwaa vikombe kumi ikifuatiwa na timu ya kanda ya Buswelu, nafasi ya tatu ikienda kwa Pasiansi na ya nne ikienda kwa kanda ya Bwiru.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.