Wanafunzi wa shule ya sekondari Buzuruga katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuitunza na kulinda miundombinu ya shule hiyo iliyogharimu zaidi ya kiasi cha shilingi milioni mia nne na sabini fedha za kutoka Serikali kuu kwa ufadhili wa benki ya dunia kupitia mradi wa SEQUIP pamoja na kutunza mazingira yake
Wito huo umetolewa na ndugu Joel Mhoja kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakati wa ziara ya ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi inayotekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo kupitia mpango wa SEQUIP ambapo amewataka wanafunzi kulinda miundombinu ya shule ili isiharibike pamoja na kuhakikisha wanapanda miti kwa ajili ya kutunza mazingira yanayozunguka shule hiyo.
‘.. Serikali inafanya jitihada ya kuhakikisha mnasoma katika mazingira mazuri, Niwaombe watoto kuilinda na kutunza mazingira pamoja na miundombinu yake kwa namna yeyote msiwe sehemu ya kuhujumu ubora wa miundombinu yetu, Alisema
Kwa upande wake mratibu wa mradi wa SEQUIP kutoka Benki ya Dunia Bi Innocent Najima Olingo amewataka wanafunzi kuzingatia masomo ili uwekezaji uliofanyika uwe na tija sambamba na kuwataka wanafunzi hao kuishukuru serikali kwa jitihada inayofanya kuwekeza katika elimu.
Mwalimu Sylvester Mrimi ambae ni Kaimu Mkurugenzi ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa utekelezaji wa mradi huo pamoja na kuahidi kufanyia kazi ushauri wote uliotolewa na wataalam hao.
Timu hiyo ya wataalam kutoka OR-TAMISEMI, Wizara ya Elimu na Benki ya Dunia imefanya ziara katika shule ya Sekondari Buzuruga, shule ya msingi Mwenge na kutembelea eneo itakapojengwa shule ya msingi Igalagala kata ya Sangabuye ambapo walitumia nafasi hiyo kuipongeza manispaa ya Ilemela kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huo uliozingatia ubora na ufanisi
Shule ya sekondari Buzuruga ilianza mwezi Mei, 2022 ikiwa na wanafunzi 368 wakike 190 na 178 wakiume wote kutoka shule za Kangaye na Nundu na mpaka sasa ina jumla ya wanafunzi 1,122, 529 wakiume na 593 wakike huku ikikabiliwa na changamoto za uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, uhaba wa vitabu, samani za ofisini na nyumba za walimu amesema Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Bertha Nkuba
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.