Wanafunzi wa Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuishi kwa kufuata mtindo bora wa maisha ili kujikinga na maradhi yanayoweza kuepukwa kwa kufanya mazoezi,kula lishe bora sambamba na kutembelea vituo vya afya mara kwa mara kufahamu hali za afya zao.
Hayo yamesemwa na Afisa lishe wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi .Pili Khasim wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Bujingwa iliyopo kata ya Buswelu ikiwa ni muendelezo wa kutoa elimu ya afya na lishe katika maadhimisho ya wiki ya lishe kitaifa.
" ...Mnapaswa kula lishe bora ninyi bado mnakuwa, kuleni mlo kamili muimarishe afya zenu na akili zenu kwa ujumla.Taifa linawategemea muwe viongozi wa kesho mtakaoweza kuiletea nchi yetu maendeleo..."
Aidha Afisa lishe huyo amewaasa wanafunzi hao kuacha kujihusisha na matumizi ya vileo mbalimbali , madawa ya kulevya na uvutaji bangi ambao madhara yake ni pamoja na kusababisha vijana kuchanganyikiwa,kupoteza uwezo wa kufikiri na kufanya vibaya kitaaluma sambamba na kujipandikizia magonjwa ya kudumu kama vile magonjwa ya moyo na figo.
Mbali na elimu ya lishe waliopatiwa, wanafunzi hao walipata fursa ya kuelekezwa na kufanya mazoezi mepesi ya viungo yatakayoweza kuimarisha miili yao.
Cecilia John ni mwanafunzi katika shule ya sekondari Bujingwa amepongeza juhudi za Manispaa kutenga muda na kuwafikia kuwapa elimu juu ya afya zao.
"...Hapa shuleni tunafundishwa vitu vingi pamoja na haya ya kiafya lakini ujio huu umekuwa wa pekee sana na kila mtu naona kama amefurahi,itachukua muda kusahau tuliyofundishwa hapa.."
Akihitimisha kusanyiko hilo Mkuu wa shule ya sekondari Bujingwa Mwl.Magweiga Chacha Magabe amewataka wanafunzi wake kuwa mabalozi wazuri kwa familia zao wanakotoka na mfano wa kuigwa kwa jamii katika kuyaishi yale yote waliofundishwa .
|
|
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.