Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela , Mhandisi Modest Apolinary amewataka wanafunzi kidato cha nne kuhakikisha wanakuwa mfano bora wa kuigwa na wenye nidhamu mara baada ya kuhitimu elimu yao ya kidato cha nne
Mhandisi Modest ametoa rai hiyo wakati wa hafla ya mahafali ya 82 ya shule ya sekondari ya wavulana Bwiru yaliyofanyika katika viwanja vya shule hiyo Oktoba 20, ikiwa ni takriban wiki tatu kuelekea mtihani wa kidato cha nne 2022
‘.. Niwaombe vijana mnaotoka hapa leo mnaingia mtaani nendeni mkawe mfano bora, mkawe na nidhamu msiende kuwa vibaka mtaani, mkawe wazalishaji wakati mkisubiri kuendelea na shule ..’ Alisema
Aidha amewataka wazazi kuendelea kuwalea watoto wao katika maadili yanayofaa mara baada ya kuhitimu mtihani wa kidato cha nne ili kujenga jamii yenye maadili na nidhamu.
Pamoja na hayo Mhandisi Apolinary amekemea vitendo vya utoro mashuleni huku akizitaka bodi za shule na walimu kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo na kushuka kwa nidhamu huku akisistiza kuwa elimu ya msingi mpaka kidato cha sita inatolewa bure na Serikali chini ya Rais Mhe Samia Suluhu Hasan, Na manispaa yake ikisaidia watoto zaidi ya hamsini walioshindwa kujigharamia huduma za kawaida hivyo hakuna sababu ya mwanafunzi kushindwa kwenda shule
Kwa upande wake makamu mkuu wa shule ya sekondari Bwiru wavulana Mwalimu Daniel Ibrahim Kitambara amesema kuwa shule hiyo ilianzishwa mwaka 1920 ikitoa elimu ya msingi na mwaka 1938 ilipanuliwa na kuanza kupokea kidato cha kwanza na kuongeza kuwa kitaaluma imekuwa ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka huku lengo kuu likiwa ni kuondoa sifuri kabisa licha ya kukabiliwa na changamoto za upungufu wa mabweni mawili, upungufu wa vitabu vya ufundi na ukarabati wa nyumba za walimu
Philipo Marco Busungu ni miongoni mwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya kidato cha nne shule ya sekondari Bwiru wavulana ambapo amewashukuru walimu wake kwa maandalizi mazuri huku akiahidi kufanya vizuri katika mtihani wake wa mwisho sanjari na kuwaomba wanafunzi wanaobaki kuendelea kuzingatia masomo na nidhamu
Sajda Halfan ni miongoni mwa wazazi wenye watoto wanaohitimu ambapo yeye amewapongeza kwa kufikia hatua hiyo pamoja na kuwataka kuendelea kuishi kwa nidhamu
Mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022 unatarajiwa kuanza tarehe 14/11/2022na kukamilika tarehe 01/12/2022 ambapo jumla ya wananfunzi 6905 kutoka katika shule za Manispaa ya Ilemela wanatarajia kufanya mtihani huo kati yao wavulana ni 3376 na wasichana ni 3529
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.