"Ili uweze kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi tunakutegemea uzingatie vitu vitatu ambavyo ni kuhakikisha unaweka mipango sahihi ya kazi, kuisimamia mipango yako vizuri, kwa kupima na kutekeleza kwa usahihi, na upimaji wa utekelezaji wa mipango yako"
Rai hiyo imetolewa na Mwalimu Sylvester Murimi Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari alipokuwa akimwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela wakati akifunga semina elekezi iliyotolewa kwa walimu wa ajira mpya na tume ya utumishi wa walimu siku ya tarehe 03 Julai, 2025
Sambamba na hilo mwalimu Sylvester amewataka walimu hao kujiepusha na kuwa chanzo cha migogoro sambamba na kuepuka mahusiano mabaya mahala pa kazi baina ya watumishi na wanafunzi kiujumla.
Aidha Bi Tabitha D. Bugemwe ambae ni afisa utumishi kutoka manispaa ya Ilemela akiongea na walimu hao amewaeleza kuwa kazi ya ualimu ni wito, hivyo anatamani kazi hii iendelee kuwa wito ndani yao pia kwasababu tupo kwenye dunia ya utandawazi hivyo kama mwalimu usipokuwa makini kama mwalimu, mzazi na mlezi, hamtaweza kuwafikisha watoto mahali ambapo wanatakiwa kufika.
"Ualimu ni wito hivyo naomba mkauishi ndani yenu wito huu wa ualimu kwa kuwa walimu bora, zingatieni sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa kila wakati katika utendaji wenu wa kazi, kulea na kusimamia vema wanafunzi kwani mwalimu ni mlezi serikali na wazazi wameawaamini na kuwakabidhi watoto muwalee na kuwaelimisha ili kujenga taifa lijalo, Tendeeni haki nafasi mlizopata kwa kufanya kazi kwa ufanisi na weledi mkiyazingatia haya mtaona kuwa utumishi wa umma ni mzuri na mwepesi " ",alisisitiza Bi Tabitha.
Nae Bi Penina Alphonce Katibu msaidizi wa Tume ya Utumishi wa walimu aliwakumbusha walimu hao kuzingatia masuala ya maadili na nidhamu kwa walimu huku akiwahimiza kuzingatia waraka wa serikali wa mavazi na kuhakikisha wanavaa mavazi ya kiutumishi.
Akishukuru kwa niaba ya wenzake mwalimu Boaz Mwambelwa ambae ameajiriwa hivi karibuni amesema kuwa yeye amekaa miaka tisa bila ajira toka amemaliza chuo, ambapo ameahidi kufanya kazi kwa bidii na ueledi na kuzingatia miiko ya ualimu.
Semina hiyo elekezi iliyoratibiwa na tume ya utumishi wa walimu ililenga kuwajengea uwezo walimu juu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo haki na wajibu, maadili na nidhamu, utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu, na masuala ya rushwa ambapo jumla ya walimu 134 wa ajira mpya wamepatiwa semina elekezi kati yao walimu 108 ni wa sekondari na 26 ni wa msingi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.