Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili wenye virutubisho vyote muhimu vya makundi ya chakula kwa ajili ya ukuaji wa binadam ikiwemo protini, wanga, vitamini, madini, mboga mboga, matunda na maji
Hayo yamebainishwa na afisa Lishe wa manispaa ya Ilemela Bi Pauline Machango wakati wa zoezi la utoaji wa elimu kwa vitendo juu ya masuala ya lishe, ugawaji wa Chanjo ya vitamini 'A' na Dawa za minyoo kwa watoto wadogo lililoendeshwa katika mitaa ya Kaguhwa kata ya Nyamhongolo na Igombe ‘B’ kata ya Bugogwa ambapo amewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto hawakosi mlo wenye makundi yote ya chakula ili kuwakinga na maradhi sambamba na kuwa kinga dhidi ya udumavu
‘.. Wapeni watoto chakula chenye mjumuisho wa makundi yote muhimu katika kila mlo, Maji hayamo katika makundi hayo lakini msiache kuwapa maana maji ndio sehemu kubwa katika mwili wa binadamu na ndio yanayosaidia makundi yote hayo yaweze kufanya kazi kwa urahisi mwilini ’ Alisema
Aidha Bi Machango amewaasa wazazi kutenga muda kwaajili ya kufuatilia ukuaji wa watoto na malezi yao badala ya kuwaachia wafanya kazi wa ndani na wasaidizi wengine wa nyumba pekee
Nae Bi Pili Kasim kutoka kitengo cha afya na lishe, amewaomba wazazi na walezi kuacha tabia ya kukatisha kuwapeleka watoto kliniki pindi wanapofikisha miaka miwili na nusu hasa baada ya kumaliza chanjo zilizozoeleka ikiwemo ile ya ugonjwa wa Surua, mlango wa kizazi, kupooza, homa ya uti wa mgongo na ile ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu
Levina Merickiad ni mtendaji wa mtaa wa Kaguhwa, amesisitiza kuwa ukosefu wa kipato isiwe sababu ya watoto kukosa mlo kamili kwani makundi yote muhimu ya chakula yanaweza kupatikana hata katika vyakula vya kawaida visivyokuwa na gharama kubwa kama mchanganyiko wa kisamvu, viazi, yai, karanga, dagaa na vyakula vyenginevyo vyenye gharama nafuu na vinavyopatikana kwa urahisi
Bi Zawadi Evarist kutoka mtaa wa Igombe ambae pia ni mzazi wa mtoto Teopister Soba Charles aliyekutwa na utapiamlo na Bi Jesca Peter mkazi wa Kaguhwa kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa elimu iliyotolewa dhidi ya kuwaandalia watoto mlo kamili pamoja na tahadhari za kuchukua ili kuwakinga na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa mlo kamili sanjari na kuahidi kufanyia kazi elimu waliyoipata kutoka kwa wataalam wa Lishe
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.