Jamii imetakiwa kuwafikisha katika hospitali ya wilaya ya Ilemela wagonjwa wenye shida ya ulemavu wa mdomo wazi ili waweze kufanyiwa upasuaji sanifu na urekebishaji bila gharama zozote, kwa muda wote ili kuwaondolea unyanyapaa katika jamii.
Rai hiyo imetolewa na Daktari Barnabas Gladson kutoka kitengo cha afya ya kinywa na meno hospitali ya wilaya ya Ilemela wakati wa zoezi la upasuaji kwa watoto wenye mdomo wazi linaloendelea kufanyika katika hospitali ya wilaya ya Ilemela ambapo amewataka viongozi wa mitaa, mabalozi na wananchi wote kwa ujumla kuwafikisha katika vituo vya kutolea huduma watu wenye mdomo wazi kwaajili ya matibabu
‘... Shida ya mdomo wazi ni tatizo linalotibika, mtoto anaweza kupata unyanyapaa mkubwa sana kama ataendelea kuwa na hili tatizo, Sasa utalaam huu umefika kwetu na huduma hii inatolewa bure na wakati wowote unapopata mtu mwenye tatizo hili mfikishe hospitali ya wilaya ya Ilemela ili apate huduma ...’ Alisema
Aidha Dkt Barnabas amesisitiza kuwa ufanikishaji wa upasuaji na urekebishaji wa mdomo wazi utasaidia watoto au wagonjwa wengine kuweza kuendelea na shughuli zao za kila siku na kufikia ndoto zao sanjari na kusisitiza kutoogopa na kuwafikisha katika vituo vya huduma watu wote watakaobainika kuwa na changamoto hiyo
Bi Frida Mtungirehi Mtachoka ni mtaalam wa huduma za usingizi katika hopsitali ya wilaya ya Ilemela ambapo amefafanua kuwa kufanyika kwa huduma hizo katika hospitali hiyo kutawaongezea uzoefu na ujuzi mpya katika kazi za kila wanazozifanya za kutoa huduma kwa wananchi huku akiwakumbusha wataalam wenzake kuzingatia na kufanyia kazi juzi mpya zinazopatikana kupitia zoezi hilo linaloendeshwa katika kituo chao
Nae Bi Elina Matata kutokea wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ambae ni mzazi wa mtoto Neila Adrian mwenye changamoto ya ulemavu wa mdomo wazi akasema kuwa amepata taarifa za uwepo wa huduma bure za upasuaji sanifu na urekebishaji wa ulemavu wa mdomo wazi kutoka katika uongozi wa serikali ya mtaa wa Buswelu pamoja na kushukuru kwa uwepo wa huduma hiyo huku akiwaomba wazazi na walezi wengine kuwafichua na kuwafikisha katika vituo vinavyotoa huduma kwaajili ya matibabu
Manispaa ya Ilemela inaendesha zoezi la upasuaji sanifu na urekebishaji wa mdomo wazi maarufu mdomo Sungura katika hospitali yake ya wilaya iliyopo eneo la Isanzu kata ya Sangabuye kwa siku zote na muda wote bila gharama yeyote kwa wananchi wa maeneo yote
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.