Walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF wamehamasishwa kuhamia katika mfumo wa kidigitali ili kurahisisha utaratibu wa malipo na kupunguza gharama za zoezi la uhawilishaji fedha na upotevu wa muda
Rai hiyo imetolewa na mratibu wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF wilaya ya Ilemela Bwana Leonard Robert wakati akizungumza na walengwa na wasimamizi wa ngazi ya jamii kutoka kata ya Buswelu ambapo amewaasa wanufaika kuhakikisha wanatumia njia za benki na mawakala huku akisisitiza wasimamizi wa ngazi ya jamii kuwaelimisha walengwa juu ya faida za kutumia mifumo ya kidijitali
‘.. Ukitumia mfumo wa kidijitali fedha yako itatoka TASAF makao makuu moja kwa moja, Wenyeviti pia mtusaidie kutoa elimu kwa wananchi maana wakati mwingine wanaanzia huko kwenu kwenye mitaa ..’ Alisema
Aidha Leonard amewataka walengwa kuvumilia changamoto chache za kimtandao zinapojitokeza na kusisitiza kuwa fedha zao ziko salama na hakuna itakayopotea kutokana na changamoto hizo
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Bulola ‘B’ Bwana Joseph Bogohe Masunga ameshauri zoezi la ulipaji wa kielektroniki kupitia benki, fedha za wanufaika ziwe zinatangulia katika akaunti za walengwa kabla ya kusaini karatasi za malipo ili kuepusha usumbufu kwa wanufaika kwenda benki na kukuta fedha bado haijaingia kwenye akaunti
Moja ya mjumbe wa kamati ya usimamizi ya jamii Bi Agnes Raymond Komba kutoka mtaa wa Bulola ‘B’ amewaasa walengwa kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya mpango ikiwemo kina mama wajawazito na watoto wadogo kuhudhuria kliniki na wanafunzi kuhudhuria masomo ili mpango huo uweze kuwa na tija na manufaa kwao
Jumla ya kiasi cha shilingi Milioni 277.59 kimehawilishwa kwa kaya 5682 ndani ya wilaya ya Ilemela katika mitaa yake yote inayonufaika na mpango ambapo kaya 1097 zikilipwa fedha taslimu mkononi kiasi cha shilingi milioni 49.52, kaya 4567 zikilipwa kiasi cha shilingi milioni 226.80 kwa njia ya benki na kwa njia ya simu kaya 18 zikilipwa kiasi cha shilingi milioni 1. 26 kwa njia ya wakala.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.