Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF wametakiwa kujitenga na vitendo vya kikatili na unyanyasaji katika ngazi ya kaya ili fedha wanazohawilishiwa ziweze kuleta tija na manufaa.
Rai hiyo imetolewa na afisa ustawi wa kata ya Nyamanoro ambae pia ndie mwezeshaji wa mpango huo katika kituo cha ofisi ya kata ya Kawekamo Bi. Deograsia Lubugo wakati wa zoezi la utoaji wa elimu (Community Session) kwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF ambapo amewataka wanufaika kutumia fedha zinazotolewa na mpango huo kwaajili ya shughuli za uzalishaji mali, kujikwamua kiuchumi, mahitaji ya shule, afya badala ya kutumia fedha hizo kunywea pombe na vitendo vyengine visivyofaa vinavyoweza kuchochea ukatili na unyanyasaji katika ngazi ya familia
‘.. Asitokee mtu akatumia fedha hizi kwaajili ya kununulia pombe, ukalewa ukaanza kumpiga mkeo, mumeo au watoto, Tumieni fedha hizi kwaajili ya shughuli za uzalishaji mali, mkifanya hivyo mtakuwa mbali na vitendo vyovyote vya kikatili vinavyoweza kufanyika ..’ Alisema
Aidha Bi Lubugo ameongeza kuwa kiasi cha jumla ya shilingi 2,571,121 kimehawilishwa katika mitaa miwili ya Pasiansi mashariki A na Pasiansi mashariki B iliyopo ndani ya kata anayoisimamia huku akishauri walengwa wanaopokea fedha taslimu mkononi kujitahidi kuhamia katika mfumo wa kupokea kidigitali kwa njia ya benki au simu ya mkononi
Bi Peruce Nkuru ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Pasiansi mashariki ‘A’ kata ya Kawekamo ambapo amewasisitiza wanufaika wa mpango huo katika mtaa wake kuhakikisha wanatumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kununulia nguo za sikukuu na kunywea pombe hasa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Pasaka na Eid
Nae Bi Mariam Mohamed ni miongoni mwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF kutoka mtaa wa Pasiansi Mashariki ‘A’ ambapo amefafanua kuwa kupitia mradi wa TASAF ameweza kupata fedha zinazomsaidia kuwekeza katika biashara yake ya ufugaji wa kuku na bata hivyo kumudu gharama za maisha ya kila siku pamoja na kuwasomesha watoto na wajukuu zake sanjari na kupata uhakika wa huduma za afya kwa kaya yake.
Jumla ya kiasi cha shilingi milioni 243.5 zimetolewa kwa kaya 5,383 ndani ya manispaa ya Ilemela ikiwa ni malipo ya kipindi cha Novemba – Desemba,2023 kwa mkupuo mmoja.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.