Walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) ndani ya manispaa ya Ilemela wametakiwa kuanza kujiandaa na ukomo wa ruzuku zilizokuwa zinatolewa na mpango huo.
Hayo yamebainishwa na mwezeshaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF kata ya Nyamanoro Ndugu Mbwana Rashid Lunga wakati akizungumza na walengwa hao kabla ya kuanza kwa zoezi la uhawilishaji fedha ambapo amesema kuwa walengwa walioingia kwenye mpango kuanzia mwaka 2021 watatakiwa kuwa wamefuzu katika mpango itakapofika mwezi Septemba, 2025 hivyo kuwaasa kujiandaa kisaikolojia, kimipango na kimkakati
'.. Tujiandae na tuwe na hizi habari kuwa itafika hatua tutafuzu katika mpango huu wa TASAF, Na itakapofika Septemba 30 mwaka huu ndio itakuwa mwisho wa ruzuku kwa walengwa walioandikishwa kuanzia mwaka 2021 mpaka viongozi wetu wa mitaa watakapotupatia taarifa nyengine mpya zitakazolewa na mpango ..' Alisema
Aidha Ndugu Mbwana amewataka wanufaika wa mpango huo kuzingatia matumizi bora ya nishati kama sera ya nchi inavyotaka ili kuimarika kiuchumi pamoja na kulinda afya zao dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya nishati zisizofaa kama ugonjwa wa macho kwa kutumia nishati ya kuni na mkaa
Kwa upande wake Bi Martha Joseph Kaloli ambae ni mnufaika wa mpango huo kutoka kata ya Nyamanoro licha ya kushukuru kwa utekelezaji wa mpango amefafanua kuwa mpango umemsaidia kujikwamua kiuchumi kwani ameweza kuanzisha miradi midogo midogo inayomsaidia katika kusomesha watoto, kulipia gharama za chakula na kuendesha maisha yake ya kila siku huku Bi Joyce Peter kutoka kata ya Ibungilo akiwaasa walengwa wenzake kutumia vizuri fedha wanazozipata kupitia mpango huo wa kunusuru kaya masikini ili mradi utakapokoma waweze kujitegemea kiuchumi
Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwa kushirikiana na Manispaa ya Ilemela umeendelea kutekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini katika mitaa yake yote 171 na kwamba fedha zimekuwa zikihawilishwa kwa walengwa mmoja mmoja huku miradi mbalimbali ikitekelezwa kupitia mpango huo kama barabara, shule na zahanati kwa lengo la kuwaondolea wananchi umasikini.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.