Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia divisheni ya afya , ustawi wa jamii na lishe inaadhimisha wiki ya lishe kitaifa kuanzia Oktoba 24 hadi 30, 2024 ikiwa na lengo la kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa jamii sambamba na kufuata mtindo bora wa maisha.
Akizungumza wakati akitoa elimu hiyo kwa wakazi wa mtaa wa Mlimani B uliopo kata ya Kirumba Afisa lishe wa Manispaa hiyo Bi.Pili Khasim amewaeleza wakazi hao kuwa wanaweza kufanya kilimo cha mboga mboga na matunda kwa kutumia vitu mbalimbali vinavyoweza kuhifadhi udongo kama vile mifuko, matairi mabovu au kutengeneza bustani ndogo kulingana na ukubwa wa eneo na kupanda kwa mpangilio mzuri.
"...ni muhimu watu wote kupata lishe bora kwa kuzingatia makundi sita ya vyakula,eneo lako dogo linaweza kuwa na tija kubwa ikiwemo na kukupunguzia gharama kubwa za kununua mboga kila siku..." amesema Bi.Pili
Pauline Machango ni Afisa lishe amewataka wananchi hao kuhakikisha wanafuatilia afya zao kwa kula mlo kamili wenye virutubisho vyote kwa viwango sahihi.
Ameongeza kuwa maradhi mengi yanaweza kuepukwa kwa kula vizuri na kufanya mazoezi na kuachana na mitindo ya maisha isiyofaa kama vile kuacha unywaji pombe uliokithiri na uvutaji wa sigara.
Aidha Bi.Pili amewakumbusha kina mama kuzingatia ulaji mzuri ndani ya siku 1000 muhimu kuanzia mimba inapotungwa mpaka mtoto anapotimiza miaka miwili huku akikitaja kipindi hicho kuwa muhimu zaidi katika makuzi ya viungo vyote vya mwili wa mtoto sambamba na akili yake.
Nae mratibu msaidizi wa chanjo Ramadhan Himay ameeleza umuhimu wa chanjo mbalimbali ikiwemo chanjo ya korona, saratani ya mlango wa kizazi,polio na chanjo mbalimbali za watoto kuanzia wanapozaliwa na kuwataka wananchi kujiepusha na imani potovu juu ya chanjo hizo.
"...Baadhi yenu mnasema chanjo zinaua nguvu za kiume,zinasababisha watoto wa kike kukosa watoto sio kweli chanjo hizi zimethibitishwa na wizara ya afya kuwa ni salama ..."
Eliada Masinde ni mtoa huduma za afya ngazi ya jamii katika mtaa wa Mlimani B yeye anajivunia kuwa mmoja wa mabalozi wazuri wa masuala mbalimbali ya afya huku akiwasihi wananchi wenzake kujipenda na kufuatilia afya zao katika vituo vya afya na sio kusubiri kuumwa.
Maadhimisho hayo yamepambwa na kauli mbiu isemayo " mchongo ni afya yako zingatia unachokula."
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.