Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la SOS children’s village linaendelea na utoaji wa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanaojitolea ,maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata ikiwa ni sehemu ya kuchochea malezi bora ndani ya familia kupitia mradi wa kuimarisha familia.
Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo mratibu wa dawati la watoto Idara ya maendeleo ya jamii Ilemela Bi.Sarah Nthangu amewataka wahudumu hao kuwa mfano wa kuigwa katika kuhakikisha kuwa wanaelewa vizuri masuala ya malezi na makuzi ya watoto na wanatoa malezi bora kwa familia zao kwani wao ndio taswira halisi ya kitakachoonekana baada ya zoezi hilo.
Akifungua mafunzo hayo kaimu meneja miradi SOS children’s village Mwanza Elizabeth Swai amesema familia zinapaswa kulea watoto wao kwa malezi bora na kuimarisha upendo kwa watoto ili kuwaondolea mawazo hasi ya kutoroka majumbani na kuleta ongezeko la watoto wa mitaani .
“..Tunawajibika kuwalea watoto wetu kwa upendo ,watoto wanapaswa kulelewa na baba na mama kwa pamoja ni matamanio ya kila mzazi na familia kwa ujumla kupata mtoto mwenye maadili mazuri..”
Nae mratibu wa mradi wa kuimarisha familia kutoka shirika hilo Bi.Kokutona Kayungi amesema yapo mafanikio mengi yaliyoonekana kwa kuwahudumia walengwa ambao ni familia zinazoishi katika mazingira hatarishi toka kuanzishwa kwa mradi huo ambapo mwaka 2024 mradi ulitekelezwa ndani ya kata nne za Kayenze,Sangabuye,Bugogwa na Shibula huku akifafanua kuwepo kwa ongezeko la kata za kuzihudumia za Kirumba,Ilemela,Buswelu,Nyamhongolo na Kahama kwa bajeti ya mwaka huu 2025.
“..Mpango wa kuimarisha familia unawawezesha kuinuka kiuchumi na kuweza kuhudumia familia zao.Tunataka jamii yenyewe iwe na uwezo wa kuhudumia walengwa ,kusaidiana na kuwezeshana wao kwa wao.”
Moses Mapolu ni miongoni mwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutoka kata ya Sangabuye katika mtaa wa Igalagala yeye anapongeza shirika hilo kwa kuona umuhimu wa kuishirikisha jamii katika masuala ya malezi na makuzi ya watoto kwa kuzingatia kuwa malezi ndiyo yanayomtengeneza mtoto kuwa anavyoonekana anapokuwa mkubwa.
Mafunzo hayo maalum yenye lengo la kupata wakufunzi walioiva kila kona ya malezi na makuzi ya watoto yanafanyika kwa siku tano mfululizo kuanzia leo 17 hadi 21 Machi 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.