Waganga wa tiba asili na mbadala ndani ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi na kuwafichua matapeli na waovu wanaojifanya waganga wa kienyeji na kusababisha mauaji
Rai hiyo imetolewa na mratibu wa tiba asili na tiba mbadala wa manispaa ya Ilemela Bi Lilian Davis Chiguma wakati wa kikao kazi cha kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu baina ya waganga wa kienyeji na wataalam wa afya wa manispaa ya Ilemela
Bi Chiguma ameongeza kusema kuwa Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria waganga wanaopiga ramli chonganishi na tiba potofu zinazochochea mauaji na kusababisha vifo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi maarufu albino
“Hakuna aliyependa kuwa albino hii imetokana na sababu za kiuumbaji za Mungu, Sasa ikitokea ukashawishika au ukashiriki katika kupanga au kushiriki mauaji yao Serikali haitakuacha salama hatua kali zitachukuliwa dhidi yako”, Alisema
Aidha Bi Chiguma akawataka waganga hao kujisajili na kufuata maadili ya tiba mbadala huku akisisitiza kuwa waganga kazi yao ni kutibu na sio kuuwa
Neema Kavishe ni afisa ustawi wa jamii anaeratibu kitengo cha watu wenye ulemavu na wazee amewataka waganga wa manispaa ya Ilemela kuhakikisha wanakuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya kikatili dhidi ya albino pamoja na kuwafichua watu wote wenye imani potofu ya kuamini kuwa kuuwa albino na kuchukua viungo vyake ni njia rahisi ya kujipatia utajiri
Kwa upande wake Mganga wa tiba asilia kutoka kata ya Buswelu Ndugu Stephano Joachim Lusana amewataka waganga wenzake kushirikiana na Serikali kupiga vita mauaji ya albino kwani vitendo hivyo vikiendelea vitatia doa waganga wengine wasiohusika pamoja na kushindwa kuendelea na utoaji wa huduma za kila siku kutokana na makatazo yanayoweza kutolewa na Serikali
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.