Kiasi cha Shilingi Milioni 12 kimetolewa kwa wafanyakazi hodari 22 wa mwaka 2023 kutoka katika Idara mbalimbali za Manispaa ya Ilemela, hayo yamebainishwa na Bi Joanitha Baltazar ambae ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la Manispaa ya Ilemela.
Fedha hizo zimetolewa kwa watumishi hao katika sherehe ya siku ya wafanyakazi Duniani zinazoadhimishwa kila mwaka siku ya Tarehe 01 Mei ikiwa ni pongezi kwao kwa ajili ya kazi bora, utii, uadilifu na kutimiza wajibu wao katika vyeo ambavyo wanavitumikia
Katika sherehe hizo ambapo kwa mkoa wa Mwanza ziliadhimishwa katika Wilaya ya Sengerema, zikiambatana na kauli mbiu isemayo “Mishahara Bora na Ajira za Stara ni Nguzo ya Maendeleo ya Wafanyakazi." Wakati ni sasa; Huku Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima ambapo aliwataka watumishi kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uadilifu, huku akiwataka waajiri kuhakikisha wanazingatia sheria za kazi kwani kinyume na hapo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao.
Katika nyakati tofauti watumishi waliotunukiwa tuzo za ufanyakazi hodari katika Manispaa ya Ilemela walikuwa na haya ya kusema;
Imelda Chundu Mtendaji wa Kata ya Mecco yeye amemshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na uongozi wa Halmashauri kwa kumuona anafaa, huku akisema kuwa anatamani sana kufanya mengi mazuri kwa kujituma na kuhakikisha shughuli za maendeleo zinafanyika kwa kiwango.
“Ninatamani sana kufanya mengi mazuri kwa kujituma zaidi katika kuhakikisha shughuli za maendeleo zinafanyika kwa kiwango kinachostahili kwa msaada wa Mungu”, amesema Imelda
Nae Musa Zuberi Afisa TEHAMA amemshukuru Mhe. Rais wa Ja,huri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji wake wa kazi ambao umekuwa chachu kwa watumishi wa chini kuchapa kazi kwa bidii zaidi ili kuendeleza nchi.
Violencea Mbakile, ambae ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini yeye amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa tuzo hiyo ya ufanyakazi hodari, pamoja na hayo amesema kuwa yeye anaamini kujituma zaidi katika kazi ikiwa ni pamoja na kufuata sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa Umma na kubwa zaidi ni kuipenda kazi yake huku akiahidi kuendelea kuitumikia nafasi yake kwa uadilifu na ushirikiano kwa watumishi wenzake.
Mkuu wa divisheni ya utawala na Rasilimali watu, Bi Leokadia Humera amewapongeza watumishi hao na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa bidi ili waweze kuwa chachu kwa watumishi wengine.
Zawadi ya Fedha na vyeti vilitolewa kwa; walimu wa shule za msingi za Kabangaja na Bulola, mwalimu kutoka shule ya sekondari Bwiru wavulana, afisa misitu msaidizi, afisa mipango (ii), mtendaji wa kata, afisa kilimo msaidizi, afisa uvuvi, afisa tehama, afisa manunuzi, afisa biashara, mkaguzi wa ndani (ii), msaidizi wa kumbukumbu, mwandishi mwendesha ofisi, mtendaji wa mtaa, mwandishi wa vikao (ii), mhasibu (ii), muuguzi kutoka kituo cha afya cha sangabuye, afisa maendeleo ya jamii mkuu, afisa afya mazingira msaidizi, mkuu wa divisheni ya elimu ya awali na elimu msingi na mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini.
Kati ya watumishi hao 22 waliopata ufanyakazi hodari, watumishi 20 walipatiwa kiasi cha Shilingi laki tano kila mmoja na watumishi wawili walipatiwa Shilingi Milioni moja kila mmoja.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.