Wafanyabiashara wasioshiriki zoezi la usafi wa kila jumamosi ya wiki la mwisho wa mwezi na waharibu wa mazingira kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kulipa faini au kufikishwa mahakamani ili kulinda mazingira yanayowazunguka na usafi wa maeneo yao
Hayo yamesemwa na afisa afya na mazingira wa manispaa ya Ilemela Bwana Peter Yohana Singu wakati wa zoezi la usafi wa kila mwisho wa mwezi lililofanyika katika soko la Kiloleli kata ya Ibungilo ambapo amesema kuwa zipo sheria zinazoelekeza jamii kufanya usafi na kulinda mazingira yanayowazunguka hivyo kitendo cha baadhi ya wafanyabiashara kujificha wakati wa shughuli za usafi na wengine kuendelea na shughuli zao hakikubali na si cha kiungwana
‘.. Hata vitabu vya dini si vinasema mtu anapokosea unamuita mara ya kwanza unamkanya, mara ya pili unamkanya, mara ya tatu hakuna tena kumkanya kwa mdomo unachukua hatua, kwa sababu ndivyo binadamu tulivyo kama kusingekuwa na sheria kila mmoja angekuwa anafanya anavyotaka ..’ Alisema
Aidha Ndugu Peter mbali na kuahidi kuwapatia vifaa vya usafi watu wa eneo hilo amewapongeza wafanyabiashara wa ndizi katika soko la Kiloleli kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kushiriki zoezi la usafi katika eneo lao pamoja na kulinda mazingira yao tofauti na wafanyabiashara wengine ndani ya soko hilo ambao wamekuwa wakifanya usafi kwa kusuasua na wengine kumuachia wakala wa eneo hilo kufanya usafi peke yake jambo ambalo si jema
Kwa upande wake katibu wa kamati ya usafi katika soko la Kiloleli Ndugu Hakeem Abdul amewasihi wafanyabiashara wa soko hilo kutekeleza agizo la serikali la kufanya usafi kwa kila mwisho wa wiki ya mwezi na kwamba usafi huo usiishie tu eneo la soko bali hata majumbani kwao wanapoishi huku akiongeza kuwa wao kama wafanyabiashara wa soko la Kiloleli wanatumia uchafu kama fursa kwani wamekuwa wakitengeneza mkaa kutokana na uchafu unaotokana na bidhaa ya ndizi
Baraka Amri ni afisa usafi na mazingira katika kata ya Ibungilo ambapo amesema kuwa suala la usafi ni la kushirikiana na kila mmoja kutimiza wajibu wake kati ya wafanyabiashara wa soko la Kiloleli na wakala wao badala ya kuachia upande mmoja wa wakala peke yake kwani wafanyabiashara wasoko hilo nao wanaowajibu wa kufanya kuhakikisha mazingira yao yanakuwa safi na salama
Joachim Mjuni na Prisca Innocent ni wafanyabiashara wa soko la Kiloleli ambapo wameshukuru kwa zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi kufanyika katika soko lao kwani limewahamasisha na kuwakumbusha wajibu wao katika kufanya usafi wa mazingira yanayowazunguka huku wakiwaomba wafanyabiashara wenzao kutopuuza suala la usafi kwani ni la faida kwao binafsi kwa kujikinga na magonjwa yakiwemo ya mlipuko kama kuharisha na kipindupindu yanayotokana na uchafu wa mazingira
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.