WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZILIZOPO WILAYANI ILEMELA KUJIENDELEZA KIUCHUMI
Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ya Ilemela Daktari Leonard Masale amewataka wafanyabishara ndogondogo kwa jina jingine wamachinga wanaopatikana katika kata zilizopo wilayani Ilemela kutumia fursa mbalimbali zilizopo wilayani humo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi.
Rai hiyo ameitoa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa kwa ushirikiano wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Integrity Foundation Society na Idara ya maendeleo ya jamii ya Manispaa ya Ilemela.
Pamoja na hayo amewataka kufatilia bajeti zinazotengwa na halmashauri kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo sambamba na kutumia fursa zote za kujikwamua kiuchumi zinazojitokeza katika maeneo yao yakiwemo mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa wilayani humo
Akisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo Afisa Maendeleo ya jamii wa Manispaa ya Ilemela ndugu Sitta Singibala amewataka wafanya biashara hao kuyatumia mafunzo waliyoyapata kuweza kukuza mitaji yao sambamba na kuongeza ufanisi wa bidhaa wanazozizalisha ili kuleta ushindani katika soko na kuyafikia malengo ya serikali ya nchi ya viwanda sanjari na uchumi wa kati.
Nae Mkufunzi wa mafunzo hayo ya ujasiriamali Bwana Isaac Mnyangi kutoka Integrity Foundation Society amewataka wafanyabiashara hao kuwa na mawazo tofauti kwa kutofikiria kuajiriwa huku akiwasisitiza juu ya kueshimu miiko ya biashara kwa kutofanya biashara kwa mazoea, “Watu waliosoma ujasiriamali wana uhakika wa maisha hivyo fikirieni tofauti na mkafanye biashara zenu kwa umakini na si mazoea”, alisisitiza.
Miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo Ndugu Allan Kasembo kutoka kikundi cha wajasiriamali wa soko la Kirumba amesema kuwa atayatumia mafunzo aliyoyapata katika kujiongezea kipato kwa kufanya biashara tofauti na awali huku akiomba uwepo wa utaratibu wa mara kwa mara wa utoaji wa mafunzo
Nao Zena Yasini na Martha James wa kata ya Pasiansi na Kirumba wameishukuru Ilemela kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa elimu za ujasiriamali katika kuwasaidia kujikwamua, kuzitambua pamoja na kuzitumia fursa zilizopo. “Tunashukuru kwa mafunzo haya yanayotolewa na manispaa yetu, tunaamini baada ya kuisha kwa mafunzo tutaweza kuzitambua na kuzitumia fursa zilizopo”, walisema.
Mafunzo haya ya ujasiriamali ni zoezi endelevu ambalo limelenga kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara ndogondogo katika masoko yote yanayopatikana wilayani Ilemela
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.