Wafanyabishara wilayani Ilemela wametakiwa kuzingatia bei elekezi ya Serikali katika uuzaji wa saruji kwa wananchi na Serikali haitamvumilia mfanya biashara yeyote atakaeenda kinyume na agizo hilo kwa kuuza bidhaa hiyo kwa zaidi ya shilingi elfu kumi na tisa na mia tano.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe Dkt Mathias Severine Lalika alipofanya ziara ya kufuatilia upatikanaji wa saruji, zoezi la uuzaji linavyoendeshwa kwa wafanya biashara wa jumla na rejareja na uzingatiaji wa sheria, miongozo na taratibu za Serikali kwa wafanya biashara wa bidhaa hiyo ambapo amekemea upandishaji holela wa bei ya bidhaa hiyo bila kuwepo kwa sababu za msingi kwani Serikali imekuwa ikitoa neema tofauti tofauti kwa wafanyabiashara wakubwa wanaochukua saruji moja kwa moja kiwandani ikiwemo kuweka kodi rafiki na kuchukua mzigo bila fedha taslimu mkononi ili waweze kuuza kwa gharama nafuu kwa wananchi
‘.. Ziara hii ni utekelezaji wa agizo la Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu alilotoa hivi karibuni kupitia Wakuu wa Mikoa baada ya kuongezeka kwa bei ya saruji hapa nchini ghafla, Kwa hiyo Sisi Ilemela tumewaelekeza bei ya ukomo isizidi 19,500 kwa wananchi ..’ Alisema
Aidha Mkuu huyo wa wilaya akawahakikishia wananchi ndani ya wilaya hiyo kuwa Saruji ipo ya kutosha kukidhi mahitaji yao huku akisisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Mhe Dkt John Magufuli inawapenda wafanya biashara na ipo tayari kuendelea kushirikiana nao katika ustawi wa nchi pamoja na kuwalinda wananchi wanyonge wanaotumia bidhaa hiyo
Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Ilemela Ndugu Saidi Kitinga akashauri wafanyabiashara hao kuzingatia bei elekezi ya Serikali kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kuongeza mzunguko wa biashara na faida hivyo kuleta tija kwa pande zote kwa maana ya wao binafsi, Serikali na wananchi kwa ujumla
Nae afisa biashara kutoka Manispaa ya Ilemela Bi Bertha George mbali na kusisitiza juu ya kuzingatia bei elekezi ya uuzaji wa saruji katika soko akapongeza wafanya biashara hao kwa kuwa na nyaraka halali za ufanyaji biashara ikiwemo leseni ya biashara na namba ya mlipa kodi, Huku afisa kutoka mamlaka ya mapato na kodi nchini TRA Bwana Rogati Joseph akihitimisha kwa kusema kuwa katika ziara hiyo amebaini upandishaji holela wa bei ya bidhaa hiyo huku akiwataka wafanya biashara wote wanaouza saruji kinyume na maelekezo ya Serikali yaliyotolewa na mkuu wa wilaya kuacha tabia hiyo mara moja kwani baada ya hapo hakutakuwa na huruma kwa mtu yeyote atakaekaidi agizo lililotolewa.
Akihitimisha mfanyabiashara Bi Khadija Said kutoka Texas Hardware ambae ndio wakala mkuu wa bidhaa ya saruji ndani ya wilaya ya Ilemela mbali na kushukuru kwa elimu aliyoipata kufuatia ziara hiyo ya kamati ya ulinzi na usalama akaahidi kuzingatia bei elekezi ya bidhaa hiyo kwa wateja wake sanjari na kuwasisitiza nao kuzingatia maelekezo ya serikali wanapoenda kuuza kwa watumiaji wa mwisho.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.