“ Ni lazima kujali usalama na usafi wa mazingira wakati na baada ya biashara,DC peke ake,ofisi ya Mkurugenzi na wataalam wake hawataweza ndo maana tumeitana hapa ili tuwe na uelewa wa pamoja kama timu tukikaribisha ushauri na maoni yenu katika kuboresha masoko yetu.”
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Hassan Elias Masala wakati wa kikao kazi kilichojumuisha Watendaji wa kata,watendaji wa mitaa,viongozi wa wafanyabiasha na wamachinga Ilemela,wataalam wa masuala ya masoko wa halmashauri kwa lengo la kushauriana na kuweka namna bora itakayowarudisha wafanyabiashara katika maeneo yao rasmi ya kufanyia biashara.
Akitoa taarifa juu ya hali ya utendaji wa masoko Afisa masoko wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi. Bertha George amesema pamoja na mafanikio mengi ambayo yamepatikana kama vile kuwepo kwa vyama vya ushirika katika masoko hali iliyowarahisishia kupata mikopo yenye riba nafuu,amazitaja changamoto ambazo ni baadhi ya wafanyabiashara kutotii sheria.
“ Changamoto kubwa kwa sasa ni wimbi kubwa la wafanyabiashara kuhamia maeneo ya barabarani na maeneo mengine ambayo sio rasmi hali inayoipa ugumu manispaa kuwafikia wote na kupata idadi halisi ya wafanyabiashara katika maboresho ya huduma mbalimbali ndani ya masoko rasmi.” Amesema Bertha
Akifafanua umuhimu wa wafanyabiashara kurudi kwenye maeneo yao Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Masala amesema ni jukumu la uongozi mzima wa wilaya kuhakikisha wafanyabiashara wote wanarudi kwenye maeneo yao rasmi yaliyotengwa kwa usalama wao.
Aidha amewataka watendaji wa kata na mitaa na wenyeviti wa mitaa kusimamia zoezi la kuwarejesha wafanyabiashara kwenye maeneo yao rasmi na kuongeza kuwa ipo miundo mbinu rafiki kwenye maeneo hayo kama vile taa kwa ajili ya nyakati za usiku ,mabanda yenye vivuli ,maji,barabara na mitaro ya maji.
“ Mtu anakaa barabarani kufanya biashara mahali ambapo ni hatarishi na viongozi wa maeneo hayo wapo hata ikitokea gari imefeli breki madhara yake ni makubwa na tutapoteza nguvu kazi ya taifa hili.Kama kuna cha kushauriana tushauriane ili tuvuke hapa lengo letu ni kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa salama wao wenyewe na biashara zao. ”
Elimu ya mlipa kodi imetolewa na mtaalam kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Meneja cha kituo cha kodi Buzuruga Musa Haruni ambae ametoa tafsiri ya kodi kuwa ni tozo ya lazima inayotakiwa kulipwa na mfanyabiashara kwa mujibu wa sheria.
Ndugu Musa amesisitiza kuwa sheria ya kodi ya mwaka 2015 inawataka wafanyabiashara kutoa risiti wanapouza bidhaa zao.Sheria hiyo pia inamtaka mfanyabiasha mwenye mzunguko wa mauzo wa shilingi milioni 1 kwa mwaka kuwa na mashine ya kieletroniki (EFD) na mwenye mzunguko chini ya kiwango hicho kuwa na vitabu vya risiti.
“ Ieleweke kwamba wafanyabiashara wote wanapaswa kulipa kodi kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ibara ya 138.Pia usipotoa risiti adhabu yake ni faini ya shilingi milioni 1.5 au asilimia 20 ya bidhaa uliyouza,kutokuwa na risiti ni kosa la jinai.”
Nae OCD wa Ilemela Afande Ignus amewaasa watendaji hao kufanya kazi kwa weledi kwa kuwaelewesha wafanyabiashara umuhimu wa wao kufanya biashara maeneo rasmi ili kujiepusha na matumizi ya nguvu yasiyokuwa ya lazima .
Mary Marwa ni Makamu mwenyekiti wa machinga Ilemela yeye ameshauri wazo liliowahi kujadiliwa la uwepo wa dawati la kupokea kero na maoni mbalimbali ya wafanyabiashara lifanyiwe kazi haraka ili kupunguza mkanganyiko kwa wafanyabiashara kwani wengi hawajui pa kupeleka maoni yao.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.