Wafanyabiashara katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kuwa na leseni za Biashara ili waweze kufanya biashara zao kwa amani pamoja na kujiepusha na mianya ya rushwa.
Hayo yamesemwa na Bi Milembe Barnabas ambae ni Afisa Uchunguzi kutoka TAKUKURU wakati wa kikao cha elimu kwa umma kilichowahusisha wafanyabiashara pamoja na wataalam wa Manispaa ya Ilemela.
“Tuko hapa kutekeleza jukumu letu la kutoa elimu kwa umma juu ya kujiepusha na mianya ya rushwa katika mchakato mzima wa utoaji wa leseni za biashara. Ni rahisi kufanya biashara kwa amani kwa kuhakikisha unakuwa na leseni ya Biashara ”Amesema Bi Milembe
Aidha Bi.Milembe ameanisha baadhi ya faida za kuwa na leseni ikiwemo kumtambulisha mfanyabiashara kisheria hivyo shughuli zako zinakuwa halali, kumuwezesha mfanyabiashara kupata huduma mbalimbali za kifedha kama vile mikopo na kukuza pato la taifa kwa ujumla.
Pamoja na hayo Bi Milembe ameziainisha baadhi ya kazi za taasisi yao kuwa ni pamoja na kuelimisha umma juu ya masuala ya rushwa,kufanya uchunguzi na uthibiti wa masuala mbalimbali katika nyanja tofauti sambamba na kuchunguza malalamiko mbalimbali ya rushwa.
Akichangia katika kikao hicho, Bi Elizabeth Swagi Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Divisheni ya viwanda,BIashara na Uwekezaji Ilemela amesema kuwa leseni ni haki ya kila mtu na hutolewa kwa kila mfanyabiashara yeyote ambae amekamilisha mahitaji yote ya kuanzisha biashara.
“Leseni ni haki ya kila mtu na inapaswa kutolewa kwa mfanyabiashara yeyote aliyekamilisha taratibu zinazohitajika za kujaza fomu na kuambatisha nyaraka mbalimbali za utambulisho wake na uthibitisho wa biashara yake.”,amesema Bi Swagi
Nae mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama “machinga”katika soko la Kiloleli ndugu Modest John ameomba elimu itolewe zaidi kwa jamii nzima ili kuleta uelewa wa pamoja wa masuala mbalimbali ya ulipaji kodi na tozo za serikali.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.