Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imeendelea kuungana na wadau mbalimbali kutekeleza mpango wa wizara ya elimu wa elimu ya watu wazima Mpango wa uwiano kati ya elimu ya watu wazima na jamii (MUKEJA) na elimu isiyo rasmi katika kutoa elimu ya ujuzi kuwawezesha wahusika kujitambua, kuishi kwa malengo,kujiinua kiuchumi sambamba na kupambana na umaskini,ujinga na maradhi.
Elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo usio rasmi, vyama na watu wazima inalenga kuhakikisha kuwa watoto walio nje ya shule hasa wasichana,wanawake na makundi mengine ambao hawajabahatika wanapata fursa ya mafunzo bora ya msingi.
Akizungumza wakati wa darasa maalum juu ya elimu uzazi na mafunzo ya namna ya kujikwamua kiuchumi kwa wasichana wa kata ya Kahama walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni Mkurugenzi wa shirika la “LIFE WITH HOPE FOUNDATION” Bi. Yunge Charles Nyanda amesema ni muhimu kwa jamii kuona umuhimu wa kuelimishana vitu sahihi vyenye tija kwa watu wote ili kujenga uelewa wa pamoja.
“Sisi tunatoa elimu ya uzazi, maadili mema, elimu ya mapambano dhidi ya unyanyasaji na ukatili kwa wanawake na watoto, tunatoa elimu ya ujasiriamali sambamba na matumizi bora ya Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).Tunaungana na serikali ya awamu ya sita kupitia mpango wake wa elimu kwa watu wazima” amesema
Nae mratibu wa mradi wa elimu ya uzazi Mchungaji Seth Johnson kutoka shirika la Fida International amesema ni muhimu kwa wazazi kuongea na watoto wao mara kwa mara kuwaelekeza juu ya mabadiliko ya miili yao bila aibu.
Mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo Selina Robert (31) ametoa shukrani kwa mafunzo hayo na kuahidi kuwa balozi mzuri wa kuendelea kutoa ujumbe kwa majirani zake mahali anakoishi.
“Mafunzo haya ni mazuri kwani nimejifunza vingi ambavyo nilikuwa sivifahamu,kabla ya mafunzo haya nilijua kuongea na mwanangu kuhusu mabadiliko ya mwili wake ni kosa ki maadili kumbe nilikuwa nakosea “amesema Selina.
Mratibu wa elimu ya watu wazima Wilaya ya Ilemela ndugu Recipitius Maghembe amesema anawashukuru wadau wote wanaoendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika mpango wa elimu ya watu wazima na kualika wadau zaidi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.