Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na wadau wa elimu imefanya kikao cha wadau wa elimu kwa ajili ya kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu Ilemela ili kuzitafutia ufumbuzi kwa ajili ya ustawi endelevu wa elimu katika manispaa hiyo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Mathias Severine Lalika amesema Halmashauri ya Ilemela imekuwa kinara toka kuanzishwa kwake kwa kufanya vizuri katika mambo mbalimbali ikiwemo elimu.
“Tunakumbuka kwamba kwa miaka mitatu mfululizo matokeo ya shule zetu za sekondari ya kidato cha pili yameonyesha ukomavu wetu wa hali ya juu.Mwaka 2017,2018 na 2019 ufaulu ulikuwa asilimia 94.69%,93.36% na 98.68% ambapo kimkoa tunashika nafasi ya kwanza na kitaifa nafasi ya 15,19 na 30.Sambamba na ufaulu mzuri wa shule za msingi mtihani wa taifa darasa la saba kwa kipindi cha miaka minne mfululizo shule zetu zinaongoza kwa ufaulu wa 94%.”
Pamoja na ufaulu mzuri zipo changamoto nyingi ambazo zinakwamisha maendeleo ya sekta ya elimu Ilemela,ikiwemo wazazi kutoona umuhimu wa kuchangia upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wakati wa mchana,utoro wa rejareja wa wanafunzi jambo linaloshusha ufaulu kwa baadhi ya wanafunzi,pia upungufu wa waalimu hasahasa wa masomo ya sayansi.
“Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela inayo mipango na mikakati thabiti ya kuhakikisha sekta ya elimu inakuwa kwa ubora,moja ya mkakati ni huu wa kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili kwa undani changamoto hizo na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuvuka tulipo “amesema.
Aidha Mkuu wa polisi Wilaya ya Ilemela SSP.Elisante Ulomi amesema kitengo chake kipo tayari kutoa ushirikiano kwa jamii ili kuboresha elimu ya watoto wa Ilemela.
“ Hatuwezi kusema kwa kupepesa macho juu ya uwepo wa tatizo la mimba za utotoni na mashuleni. Jamii nzima tuungane katika kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za matukio hatarishi kwa watoto wa shule.”amesema
Aidha ameonya vikali juu ya kuwepo kwa wimbi la wanafunzi wanaotumia madawa ya kulevya kama vile bangi ambayo ni hatari kwa afya na maisha yao.Ni wajibu wetu kufatilia na kutoa elimu ya msaada kwa wanafunzi ili wajiepushe na matumizi ya madawa ya kulevya .
Ndugu Ulomi amesisitiza walimu kufuatilia kwa karibu mienedo ya watoto mashuleni ili kubaini vitendo viovu vya ulawiti kwa wanafunzi huku akiwakumbusha viongozi wa dini kuwa wanayo nafasi kubwa sana katika kuelimisha na kukemea uovu huo ndani ya jamii kwa kurudisha vipindi vya dini mashuleni ili wanafunzi wawe na hofu ya Mungu.
Naye mwakilishi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) kwa Wilaya ya ilemela alisema kuwa walimu wote wajaliwe ili na wao watekeleze majukumu yao vizuri huku akitoa pongezi kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo la Ilemela Dkt. Angelina Mabula kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi kupandisha madaraja ya walimu.
“Jumla ya walimu 519 wamepandishwa madaraja kwa mwaka 2019/2020 na zoezi linaendelea kwa ufatiliaji wa karibu. CWT kwa kushirikiana na idara ya elimu inaendelea kuhakikisha walimu na wanafunzi wanakuwa mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia katika morali ya kazi.Tunata walimu tupende kazi zetu na watu wengine ndani ya jamii yetu watamani kuwa walimu.”
Kadhalika naye mwakilishi kutoka taasisi ya fedha NMB amesema wao ni wadau wakubwa katika masuala ya elimu nchini na katika bajeti zao wamejikita zaidi katika kutoa misaada ya madawati pamoja na kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule hususan katika hatua za kupaua.
Akihitimisha kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Lalika alisisitiza juu ya kuendelea kujikinga na ugonjwa wa COVID-19.
“Ndugu zangu wana Ilemela naomba muendelee kunawa mikono mara kwa mara,kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima,kutembea na vitakasa mikono na kuzingatia maelekezo mengine ya wataalam wa afya”alisisitiza.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.