Afya ya uzazi ni hali ya kuwa salama, kimwili, kiakili na kijamii na sio tu hali ya kutokuwa na ugonjwa au ulemavu katika masuala yote yanayohusiana na afya, mfumo wa uzazi na utendaji kazi wake.
Zipo changamoto mbalimbali zinazowakumba wajawazito ikiwa ni pamoja na kuchelewa kufanya maamuzi kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupata huduma, ushiriki mdogo wa wanaume katika huduma za afya ya uzazi pamoja na huduma za uzazi wa mpango, wajawazito kuchelewa kuanza kliniki upungufu mkubwa wa damu kwa kinamama wajawazito, matumizi ya dawa za kienyeji kwa ajili ya kuongeza uchungu pamoja na ukosefu wa damu salama.
Kufuatia changamoto hizo, shirika la JHPIEGO kupitia mradi wa TCI Tupange Pamoja kwa kushirikiana na idara ya afya katika Manispaa ya Ilemela iliamua kuanzisha mradi ambao umejikita katika kutekeleza afua za afya ya uzazi hasa ikilenga huduma za uzazi wa mpango na afya ya uzazi kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.
Dhumuni kubwa likiwa kuweka nguvu ya pamoja ili kuwafikia wateja wengi wanaohitaji huduma za Afya ya uzazi na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na changamoto za uzazi na vifo vya watoto ikiwa ni pamoja na kuijengea jamii uelewa juu ya maana ya afya ya uzazi.
Ili kuweza kupata mafanikio katika mradi huo Idara ya Afya manispaa ya ilemela kwa kushirikiana na TCI Tupange pamoja iliwakutanisha wadau mbalimbali katika kikao cha pamoja kwa lengo la kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga katika Manispaa ya Ilemela.
Katika kikao hicho ambacho kiliendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika, aliwataka wadau waliofika hapo kusaidiana katika kubaini sababu au vyanzo vinavyosababisha vifo vya mama na mtoto ili kuweza kuisaidia jamii ya wana Ilemela na watanzania kwa ujumla.Huku akitoa wito wa kuwataka wote waliohudhuria kikao hiki kwenda kuwa mabalozi katika jamii.
Wadau mbalimbali waliweza kuchangia huku wakishauri kuwa ili kuboresha suala zima la afya ya uzazi Mganga Mkuu aendelee kufanya usimamizi wa karibu kwenye vituo vya kutolea Huduma za uzazi ili kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinakuwa na mazingira mazuri ya kutolea Huduma kwa kuwa na Huduma bora pamoja na vifaa na madawa ikiwemo wahudumu wa Afya kuwa na kauli nzuri kwa wajawazito. Manesi wapewe semina juu nya namna bora ya kuwahudumia wajawazito ikiwemo kuwa na mavazi maalum ya kazi kama ilivyokuwa zamani.
Pamoja na hayo wote kwa umoja wao walikubaliana kuwa suala la afya ya uzazi likawe agenda ya msingi ya kudumu katika vikao vyote kuanzia ngazi ya mtaa.
Charles Marwa ambae ni Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilemela alitoa taarifa kuwa maelekezo yametolewa na Serikali kwa Wakunga kutengewa Bajeti ili wawe wanapatiwa fedha kwa kila mjamzito wanayempokea na kumpeleka kwenye kituo cha Afya. Huku akitolea maelezo kuhusu suala la ukosefu wa damu kwa wajawazito, kwa kuwataka wajawazito kuzingatia suala la lishe bora ili wapate damu ya kutosha.
Manispaa ya Ilemela ina jumla ya vituo 60 vya kutolea huduma kati ya hivyo 35 vinatoa huduma ya afya ya uzazi ambapo kati ya vituo hivyo 20 ni vya serikali na 15 ni vya binafsi pamoja na mashirika ya dini.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.