VITUO VYA AFYA NA ZAHANATI ILEMELA KUFANYIWA UKARABATI KUPITIA MRADI WA IMPACT
Mradi wa IMPACT (Improving Access to Maternal and Newborn Health in Mwanza) uliotambulishwa katika Manispaa ya Ilemela unatarajiwa kukarabati vituo vya afya na zahanati ambapo majengo ya upasuaji na uzalishaji katika kituo cha afya Buzuruga, na zahanati za Igogwe na Luhanga yatafanyiwa ukarabati, hayo yalibainishwa na afisa mwandamizi wa mradi huo Bi Edina Selestine wakati wa utambuisho wa mradi huo.
Halikadhalika mradi huu umelenga kuwafikia zaidi ya watu laki sita kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuanzia Serikali kuu hadi Serikali za mitaa.
“Manispaa ya Ilemela ipo tayari kwa utekelezaji wa mradi huu na ndio maana mliposema mnakuja hakukuwa na mlolongo wa utekelezaji wake” , Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Ndugu John Wanga wakati akifungua Mafunzo ya mradi huo.
Aidha ameushukuru mtandao wa maendeleo wa Aga Khan kwa kuletwa kwa mradi huo na kuwahakikishia kuwa Manispaa yake iko tayari kwa utekelezaji wa mradi huo huku akiwakaribisha wadau wengine wa maendeleo katika Manispaa yake.
Nae Mganga mkuu wa Manispaa Ilemela Daktari Florian Tinuga amesema kuwa mradi huo umekuja muda muafaka kwa kwenda sambamba na jitihada za Serikali za kuhakikisha vifo vya mama wajawazito na watoto vinapungua kwa kuboresha miundombinu ya afya sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mheshimiwa Renatus Mulunga, akifunga mafunzo hayo, amewahakikishia utekelezaji wa haraka wa makubaliano yote yaliyofikiwa kupitia kikao cha ufunguzi wa mradi huo.
Mradi huu wa miaka mitano unaoendeshwa na mtandao wa maendeleo wa Aga Khan kwa ufadhili wa Watu wa nchi ya Canada kwa kushirikiana na Serikali kuu, lengo lake ni kuhakikisha kuwa unapunguza vifo kwa mama wajawazito, kuongeza miundombinu ya huduma za afya na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.