Vitabu 240 vya muongozo wa elimu ngazi ya msingi na sekondari vimezinduliwa na kutolewa kwa walimu wakuu na wakuu wa shule za Msingi na Sekondari za Manispaa ya Ilemela.
Akizindua vitabu hivyo, Ndugu Saidi Kitinga ambae amemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amesema kuwa lengo kubwa la miongozo hii ni kuzitatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu ambazo Wizara ya Elimu imezibainisha.
“Wizara ya Elimu imeziona changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na kutoa vitabu vya miongozo hii ya mkakati wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu msingi na changamoto katika uboreshaji elimu msingi na sekondari kama zana ya kupambana na changamoto hizo”. Amesema Said Kitinga
Ndugu Kitinga ameongeza kusema kuwa miongozo hii inaenda kurahisisha utendaji wa walimu katika shughuli za ufundishaji jambo ambalo litapelekea kuwa na mwelekeo mzuri kielimu lakini pia itafungua njia katika kupambana na umaskini ambao ni moja kati ya maadui wa maendeleo.
Pamoja na hayo amewapongeza walimu na uongozi mzima wa Manispaa ya Ilemela kwa kazi nzuri ya maboresho ya kitaaluma inayoendelea huku akisisitiza kusimamia vizuri malengo yaliyowekwa ili kuweza kupata matokeo bora.
Nae Afisa Elimu Sekondari, Ndugu Sylvester Murimi amebainisha kuwa miongozo hiyo itatolewa kwa shule zote za Msingi na Sekondari ndani ya Manispaa ya Ilemela ili kuweka usawa katika utendaji na kuongeza ushindani kitaaluma.
“Miongozo hiyo itawafanya walimu kujiimarisha zaidi katika program zilizopo na zilizoongezwa nchi nzima bara na visiwani”, Jamila Khalfan Afisa Taaluma Msingi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.