Viongozi wanawake wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona unaosababishwa na virusi vya Covid-19 kwa kuelimisha familia zao na jamii inayowazunguka juu ya athari za ugonjwa huo na namna ya kujikinga.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na viongozi wanawake kutoka kata 19 za manispaa ya Ilemela katika ukumbi wa Monarch Hotel juu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona ambapo amewataka wanawake hao kuhakikisha wanachukua hatua mbalimbali za kujikinga na ugonjwa huo sanjari na kukinga familia zao na jamii inayowazunguka kwa kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya ili kuzuia ugonjwa huo kuenea zaidi
‘.. Kwasababu nyinyi ni wana Ilemela na ni viongozi ambao tunatarajia mpate elimu na muifikishe katika jamii inayowazunguka, Kwahiyo katika hili kongamano lengo letu ni kuwapa elimu ya tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa Corona ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amewataka wanawake hao kuhakikisha wanazuia watoto waliopo majumbani kuzurura ovyo, kukaa katika mikusanyiko, kuchangia vyakula kwa njia ya mdomo ili kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa upande wake mwakilishi wa mganga mkuu wa manispaa ya Ilemela, ambae pia ni mratibu wa elimu ya afya kwa jamii Bi Rose Nyemele ametaja dalili za ugonjwa wa Korona ikiwemo kikohozi kikavu, mafua makali, kuumwa na kichwa, kutapika na kupumua kwa shida,
Nae Bi Stella Mbura ambae ni afisa ustawi wa jamii manispaa ya Ilemela akitaja njia za kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kutokaa katika mikusanyiko ya watu wengi, kunawa mikono na sabuni kwa maji yanayotiririka, kujizuia na safari zisizo za lazima.
Moja ya viongozi waliohudhuria kongamano hilo kutoka kata ya Kahama Bi Bertha Nicholous ameishukuru taasisi ya Kivulini, manispaa ya Ilemela, Benki ya Azania na ofisi ya mbunge wa jimbo la Ilemela kwa kuendesha kongamano hilo la elimu ya Korona na ujasiriamali katika kumkomboa mwanamke kiuchumi.
Akihitimisha kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ndie mkuu wa idara ya ardhi na mipango miji Ndugu Shukran Kyando amewataka wanawake hao mbali na kuchukua tahadhari za ugonjwa wa Korona kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu za mipango miji sambamba na kupima maeneo yao na kuyamiliki kisheria ili kujiepusha na migogoro ya ardhi inayotokea baada ya familia kutengana au kufariki mmoja wapo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.