Kamati ya kudhibiti Ukimwi wilaya ya Ilemela imewataka viongozi wa madhehebu ya dini kwaajili ya kusaidia kupunguza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi vya ugonjwa wa ukimwi (WAVIU)
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambae pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe. Manusura Lusigaliye wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kufuatilia shughuli mbalimbali zinazotekelezwa chini ya kamati hii katika udhibiti wa ugonjwa huo ambapo amesema kuwa ipo haja ya kuwashirikisha viongozi wa dini katika kupunguza dhana potofu zinazochangia kuacha matumizi ya dawa na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na ugonjwa huo
‘... Tutumie rasilimali zetu zote kuhakikisha tunawasaidia watu hawa, tunazo fedha tunazotenga kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma juu ya ugonjwa huu, Tuzitumie fedha hizo kwaajili ya kuwaelimisha wananchi wetu, lakini pia tusiache kuwatumia viongozi wa dini kwaajili ya kupunguza unyanyapaa ...’ Alisema
Aidha Mwenyekiti huyo ameshauri kuhamasishwa kwa vikundi vya WAVIU vilivyopo ndani ya Manispaa ya Ilemela kuchangamkia fedha za mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu zinazotolewa kulingana na makusanyo ya mapato ya ndani sanjari na kutengwa kwa ruzuku isiyorejesheshwa kupitia kamati ya Ukimwi itakayosaidia vikundi vya WAVIU vinavyofanya vizuri huku akitolea mfano wa kikundi cha LWIDIMA Group kilichopo kata ya Nyamanoro kinachojihusisha na shughuli za uzalishaji wa bidhaa Lishe
Nae mjumbe wa kamati hiyo ambae pia ni diwani wa viti maalum kutoka kata ya Nyamhongolo Mhe Saphia Mkama akaomba kukamilishwa kwa ujenzi wa majengo ya Zahanati ya Nyamhongolo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kiafya kwa WAVIU sambamba na kuzingatia suala la usiri pindi wateja hao wanapofuata huduma kituoni hapo
Kwa upande wake Ndugu Sitta Singibala aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela akafafanua kuwa manispaa imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya vikundi vinavyojihusisha na uzalishaji mali hivyo si vibaya kwa vikundi vya WAVIU navyo kuomba fedha hizo japo vipo vigezo na masharti ikiwemo umri kwa vijana na jinsia kwa watu wazima ingawa kamati ina uwezo wa kutenga ruzuku ambayo haina kigezo chochote na hairejeshwi kwa ajili ya kuwakwamua wananchi hao
Moja ya mwana kikundi cha Lwadina kilichopo kata ya Nyamonoro kinachosimamiwa na taasisi ya Shaloom Bi Joanitha Deus ameishukuru kamati ya kudhibiti Ukimwi ya wilaya ya Ilemela kwa kukitembelea kikundi chao sanjari na kuahidi ushirikiano na Serikali katika kutatua changamoto zinazo wakabili huku akisisitiza kuwa muathirika si sababu ya kutojihusisha na shughuli za kujiondolea umasikini
Kamati ya Ukimwi robo ya pili kwa Mwaka wa fedha 2020/20212 Manispaa ya Ilemelailifanya ziara katika taasisi ya Shaloom Care House Nyamanoro, Kikundi cha akina mama wanaoishi na virusi vya ukimwi kiitwacho LWIDINA Nyamanoro, zahanati ya ELCT Nyakato na zahanati ya Nyamhongolo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.