Viongozi wa dini wametakiwa kuiunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuhakikisha wanaelimisha waumini wao juu ya umuhimu wa kuchanja na kuchukua tahadhari kwa kufuata ushauri unaotolewa na wataalam wa afya.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala wakati wa kikao kazi na viongozi wa dini kilichofanyika katika ukumbi wa manispaa ya Ilemela kwa lengo kukumbushana juu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo amewataka viongozi hao kwenda kwa waumini kutoa ufafanuzi juu ya umuhimu wa kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo
“.. Serikali inao wajibu wa kuwalinda na kuwachunga wananchi wake kimwili, Lakini nyie wenzetu mnao wajibu wa kuwachunga kiroho hivyo mtagundua kazi tuliyonayo ni moja, Ni wajibu wetu kuwalinda watu hawa kwa namna yeyote ile ...’ Alisema
Aidha Mhe. Masala mbali na kuwataka viongozi hao kumshukuru Rais Mhe Samia Suluhu Hasan kwa kugharamia chanjo zinazotolewa bure kwa wananchi amewaomba viongozi hao kuhakikisha wanashiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi kikamilifu ili kusaidia utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayopangwa na Serikali kwa kuhamasisha waumini wao kujitokeza na kuhesabiwa wakati utakapofika sanjari na kuwaomba kuzingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa ibada kwa kutokusababisha kelele kwa wananchi wengine
Nae Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula alisistiza suala la wote kuwa na kauli moja ya kuwa na nia thabiti ya kuhakikisha tunajikinga na korona na kuwa suluhu iliyofikiwa kwa sasa ni kupata chanjo,
Aliongeza kusema kuwa wananchi hawajazuiliwa kujifukiza na kuwa chanjo ni hiari ila akili yako ikufikishe mbali kwani Taifa haliwezi kuwa salama kama kuna wengine hawajafikia kinga iliyofikiwa
“Kama wana ilemela tuungane na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha tunadumu katika maombi Mungu atuepushe na gonjwa hili, tupate chanjo, tusaidiane kutoa elimu juu ya ugonjwa huu”, Alisisitiza
Askofu Dkt Robert Bundala ambae ni mratibu wa kamati ya Amani ya mkoa akichangia katika mkutano huo amehimiza kuwa ni vyema kuelezana ukweli kuwa unapochelewa kupata chanjo unakaribisha kifo.
Nae Shekh Hasan Yasin Mchondo kutoka kata ya Kiseke mbali na kuipongeza Serikali na viongozi wake kwa hatua wanazochukua katika kupambana na ugonjwa huo wamewataka viongozi wenzao wa dini kuungana na Serikali katika kutoa elimu na kuhamasisha waumini juu ya umuhimu wa chanjo huku wakiahidi kuwa mstari wa mbele kwa hao wenyewe kujitokeza na kuchanja lakini pia kuhamasisha wengine kuchanjwa.
Katika kuhitimisha mkutano huo Mganga mkuu wa Manispaa ya Ilemela, Daktari Samson Marwa amewatoa hofu viongozi hao wa dini na kuwaeleza kuwa Serikali kupitia wataalam wake wa ndani imefanya utafiti wa kina juu ya chanjo hiyo, hivyo kuwaomba kujitokeza kwa ajili ya kuchanja na kusisitiza kuwa kila kata imepatiwa chanjo za kutosha kwa ajili ya wananchi wa eneo husika
“Jilinde nikulinde UVIKO-19 unazuilika, kachanje sasa”
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.