VIKUNDI VYA WANAWAKE NA VIJANA ILEMELA VYAHIMIZWA KUTUMIA MIKOPO KWA MALENGO YALIYOKUSUDIWA
Vikundi vya ujasiriamali vya Wanawake na vijana katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela vimetakiwa kuzitumia fedha walizokopeshwa kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa pamoja na kurejesha kwa wakati. Hayo yalisemwa na Mstahiki Meya Mhe.Renatus Mulunga wakati wa zoezi la utoaji wa mikopo.
“Fedha hii ambayo mmekopeshwa ikafanye shughuli za kimaendeleo na sio vinginevyo ili kuweza kurejesha kwa wakati”.Alisisitiza Mstahiki Meya
Nae Mwenyekiti wa kamati ya huduma za kiuchumi, Mhe Sarah Ngh’wani aliwasisitiza wanufaika wa mkopo huo kwa kuwataka wakazitumie fedha hizo katika kuendeleza miradi iliyopo na sio kuanzisha miradi mipya.
Aidha aliwashauri kuwa vikundi viwe na miradi ya pamoja kama vile ufugaji, kutengeneza matofali na kuongeza kwa kusema kuwa hata ile fedha Tsh.Mil.50 ya Mheshimiwa Rais itatolewa kwa vikundi vyenye miradi inayofanya vizuri.
Katika zoezi hilo la utoaji wa mikopo, vijana walihimizwa suala zima la uaminifu kwa kuwasihi kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwezesha vijana wengine kupata mikopo, hayo yalisemwa na katibu wa vijana CCM Mkoa wa Mwanza Bi Mariam Abdallah aliyehudhuria hafla hiyo fupi.
Nae mwakilishi wa vikundi vya vijana vilivyopatiwa mikopo hiyo wakati akitoa shukurani kwa kupatiwa mikopo hiyo, aliwasilisha ombi la kuanzishwa kwa mabaraza ya vijana ili kuweza kupata sehemu ya kusemea matatizo pamoja na kutoa mawazo yao.
Jumla ya fedha kiasi cha Tsh. Milioni 70 zilitolewa kwa vikundi 35 ambapo vikundi 29 ni vya wanawake na vikundi 6 ni vya vijana kutoka katika kata 19 za Manispaa ya Ilemela ambapo zoezi hilo la utoaji wa mikopo lilitanguliwa na mafunzo ya siku moja kwa vikundi vilivyokidhi vigezo lengo ikiwa ni kuwafunza namna ya matumizi bora ya mikopo na urejeshwaji wake.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.