VIKUNDI MBALIMBALI VYA UJASIRIAMALI WILAYA YA ILEMELA VYAPATIWA MAFUNZO
Shirika la Viwanda vidogo vidogo SIDO mkoa wa Mwanza limetoa mafunzo ya Ujasiriamali kwa vikundi mbalimbali vilivyopo wilaya ya Ilemela ikiwa ni mkakati wa utekelezaji na ufikiaji wa sera ya Serikali ya awamu ya tano yakuifikia Tanzania ya viwanda.
Mafunzo hayo yalitolewa kwa kushirikiana na Manispaa ya Ilemela, benki ya Posta, mamlaka ya chakula na dawa TFDA, mamlaka ya mapato nchini TRA, shirika la viwango TBS, jukwaa la biashara la wanawake TWCC, jukwaa la biashara , viwanda na kilimo TCCIA kwa ufadhili wa asasi isiyokuwa ya Serikali ijulikanayo kama TLED
Aliyekuwa mgeni rasmi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela ndugu John Wanga amekuwataka wajasiriamali waliohudhuria mafunzo hayo kuongeza ubunifu na ugunduzi ili kuongeza ubora wa bidhaa zao katika kupambana na mahitaji ya soko ili kuendana sambamba na ufikiaji wa malengo ya serikali ya Mheshimiwa Rais John Magufuli ya nchi ya viwanda.
‘… Leo Tanzania imekuwa ni jalala la kupokea vitu hata vya kawaida kabisaa kutoka nchi za jirani zetu, kutoka nchi za China, Thailand na Malasia tunapokea bidhaa zao hata kiberiti, Hivi Kibiriti cha Kangaroo kilikuwa kinatoka wapi?, Hivi sisi tunashindwa kutengeneza hata Kiberiti?, Njiti za kuchokonolea meno zinatoka wapi?, Lakini mfanyabiashara anakwenda kuchukua fedha kutoka benki alafu anaagiza mzigo anatuletea hapa, Sasa Mheshimiwa Rais kasema hapana lazima tuanzishe utaratibu wa kuwa na viwanda …’ Alisema
Nae meneja wa SIDO Mkoa wa Mwanza ndugu Bakari Songwe amesema kuwa wameanzisha kampeni ya pamoja kwa kushirikisha sekta binafsi na sekta ya Umma zilizopo ndani ya mkoa Mwanza inayojulikana kwa jina la ‘AMSHA KIWANDA’ lengo ni kutekeleza kwa vitendo adhma ya Serikali ya Tanzania ya viwanda kwa kuwasaidia wajasiriamali wadogo kufikia malengo yao kwa kuwakutanisha na wadau wote muhimu wa biashara wanazozifanya ili kuweza kukidhi mahitaji ya soko na ushindani.
Kwa upande wake mwenyekiti wa jukwaa la wanawake na uwezeshaji kiuchumi kutoka wilaya ya Ilemela Bi Winfrida Mgendi mbali na kushukuru kwa uzinduzi wa mafunzo hayo yatakayowasaidia wanawake kiuchumi kupitia vikundi vyao vya ujasiriamali amewataka kuitumia vizuri fursa hiyo iliyojitokeza kama chachu ya kukuza biashara zao na kujikwamua kimaisha kwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu huku akisisitiza kutokaa nyumbani pale wanaposikia fursa mbalimbali zinapotokea
Akihitimisha mafunzo hayo meneja wa taasisi inayofadhili mradi huo ya TLED ndugu Nelson Musikwa amesema kuwa taasisi yake imekuwa ikishirikiana na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuisaidia jamii katika kufikia malengo ya serikali hivyo mradi wa ‘AMSHA KIWANDA’ ndio mradi mkubwa wanaoutekeleza kwa sasa utakaodumu kwa miaka mitano nakuwataka wananchi na wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.