Vijana 35, wasichana 34 na mvulana mmoja wamehitimu mafunzo ya ushonaji na elimu ya jinsia yaliyokuwa yakitolewa na chuo cha ufundi stadi Nyakato kwa ufadhili wa shirika lisilo la serikali la SOS Children Mwanza pamoja na kukabidhiwa vyerehani ili kujiajiri na kujikwamua kiuchumi
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo katika ukumbi wa ofisi ya kata ya Kayenze kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Bi Neema Semaiko amelipongeza shirika hilo kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya manispaa yake pamoja na kuwataka vijana hao kutumia mafunzo waliyoyapata kujiendeleza kiuchumi huku akikemea uzembe kwa baadhi ya vijana wasiotaka kufanya kazi na kukimbilia kwenye michezo ya kubashiri ili kupata fedha kiurahisi
‘.. Hapa duniani hakuna anaekupa pesa ya bure zaidi ya kukufanya wewe ufikiri unapewa pesa kirahisi kwa kubeti kumbe ndo mpaka kile kidogo ulichonacho kinaondoka, Wazazi tusikae kimya hata ukiangalia hapa katika wahitimu wasichana 34, mvulana mmoja maanake wanaona kama kazi ya ushonaji ni ya kike ..’ Alisema
Aidha Bi Semaiko amewataka vijana katika jamii kuacha kuchagua kazi sanjari na kutumia kila fursa inayopatikana katika jamii kuondokana na umasikini
Kwa upande wake mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii manispaa ya Ilemela Ndugu Mohamed Atiki amelipongeza shirika la SOS Children kwa mradi huo huku akiyataka mashirika mengine kuiga mfano wake na kutekeleza miradi yenye tija ya moja kwa moja kwa jamii
Nae kaimu meneja wa miradi wa shirika la SOSO Children Bi Elizabeth Swai akasema kuwa vijana waliohitimu mafunzo hayo wametoka katika mitaa ya kata ya Kayenze na kwamba jumla ya kiasi cha shilingi milioni ishirini na sita zimetumika kugharamia mradi huo ikiwemo gharama za walimu wa mafunzo kutoka chuo cha Nyakato shilingi milioni saba, ununuzi wa vyerehani 35 kwa shilingi milioni kumi na tano na laki mbili na hamsini, vitambaa vya kujifunzia majora kwa shilingi milioni tatu na laki tano
John Lucas, Senora Phabian na Jalaki Yahya ni miongoni mwa wahitimu wa mafunzo hayo ambapo wamelishukuru shirika kwa kuwapa ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuacha kuwa wategemezi huku wakiahidi kutunza vyerehani walivyokabidhiwa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.