Watendaji wa kata na mitaa wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela, wametakiwa kuhakikisha wanasimamia suala zima la ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao ya utawalaili kuhakikisha halmashauri inafikia lengo lake.
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi Ummy Wayayu alipokutana na watendaji hao katika kikao kazi kilichohusu suala zima la ukusanyaji wa mapato siku ya tarehe 15 Januari 2025.
Aliendelea kuwasisitiza kuwa jukumu moja wapo la utendaji wao linahusu ukusanyaji wa mapato, bila kukusanya mapato maana yake hakuna kazi, shughuli zote za maendeleo hazitawezekana na hata ustawi wa watumishi hautawezekana, na kuwakumbusha kuwa wao ni watu muhimu sana katika eneo hili la ukusanyaji wa mapato
“Kasimamieni ukusanyaji wa mapato katika maeneo yenu ya utawala na kila mmoja wenu atimize wajibu wake kwa ueledi na uadilifu wa hali ya juu na kwa mtendaji ambae ataenda kinyume na maelekezo sitasita kuwachukulia hatua na kwa mwenye changamoto yoyote ahakikishe anaiwasilisha kwangu”,amesema Bi Ummy
Aidha amewakumbusha watendaji kuwa ni wajibu wao kuwatembelea wafanyabiashara kwa ajili ya kufuatlia kama wamekidhi mahitaji pamoja na kutoa msaada kwa wafanyabiashara ambao hawana uelewa wa namna ya kulipa tozo mbalimbali, lakini si hilo tu kuwapa uelewa juu ya namna ambavyo kodi hizo zinasaidia katika maendeleo ya nchi.
Herbert Bilia ni mchumi wa manispaa yeye amewataka watendaji hao kuhakikisha wanazingatia matumizi ya sheria ndogo za halmashauri katika suala zima la ukusanyaji wa mapato, huku Ndugu Kefadan Gembe ambae ni Afisa Biashara wa manispaa yeye amesisitiza juu ya suala la kuhakikisha kila mtendaji anakuwa na kanzidata sahihi yenye vyanzo mbalimbali katika maeneo yao ili kurahisisha zoezi hilo.
Nae Bi. Mariam Mshana, mweka hazina wa manispaa ya Ilemela, amewataka watendaji kutumia kauli nzuri pamoja na kutoa huduma bora pindi watakapokuwa wanaendesha zoezi hilo kwani ukusanyaji wa mapato unahitaji hekima kubwa
Nao watendaji hao katika nyakati tofauti wameshukuru kwa kikao kazi hicho na kupokea maelekezo yaliyotolewa ambapo wameomba kupatiwa mafunzo mbalimbali juu ya masuala ya ukusanyaji wa mapato, sambamba na kuomba uwepo wa kikao kazi kama hiki kila mwezi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika mwaka wa fedha 2024/2025 imepanga kukusanya cha shilingi bilioni 14.95 kutoka vyanzo vya ndani vya mapato fedha hizi hutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo sambamba na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za taasisi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.