Mapema leo tarehe 20 Oktoba 2025, timu ya madaktari bingwa na bingwa bobezi wa Rais Samia wamewasili Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Ilemela ikiwa ni awamu ya nne toka kuanza kwa huduma hizi.
Dkt Delfina Mkenda (Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake na ukunga) ambae ni kiongozi wa timu hiyo madaktari amesema kuwa wamejipanga kutoa huduma bora kwa wananchi wa Ilemela ili kuweza kutimiza lengo la Dkt Samia la kusogeza huduma karibu na wananchi.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi Ummy Wayayu, amemshukuru Rais Samia kwa kuweka utaratibu huu wa kusogeza karibu huduma za kibingwa na bobezi katika maeneo mbalimbali ya nchi hususan Ilemela kwani wananchi wanahitaji sana huduma hizi za kibingwa na bobezi ambapo ameahidi kutoa ushirikiano kwa madaktari hao
"Wananchi wana uhitaji wa huduma hizi ukizingatia hali ya upatikanaji wake na hali zao za kiuchumi inakuwa ni changamoto lakini timu kama hii inapokuja inakuwa ni nafuu kwao wanapata huduma hizi kwa karibu, hivyo nimshukuru Mhe Rais Dkt Samia kwa kuweka utaratibu huu wa kuwafikia wananchi wake", amesema Mkurugenzi Ummy.
Sambamba na hilo, Mkurugenzi Ummy amemuelekeza mganga mkuu wa manispaa ya Ilemela, Dkt Maria Kapinga kuweka utaratibu mzuri wa kuwafikisha wagonjwa wenye uhitaji wa huduma katika hospitali ya wilaya ya Ilemela kutokana na umbali wa hospitali hiyo ili kuhakikisha lengo lililokusudiwa la kuwapatia huduma hizo wananchi linafanikiwa.
Kambi hii ya madaktari itatoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali ya Wilaya ya Ilemela iliyopo Isanzu kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 20 hadi 24 mwezi huu wa oktoba, ambapo huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma za magonjwa ya wanawake na ukunga, watoto na watoto wachanga, upasuaji, magonjwa ya ndani na huduma za kinywa na meno.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.