Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hasan Masala amewataka makarani pamoja na wasimamizi wa maudhui na TEHAMA katika Wilaya ya Ilemela kuhakikisha wanakuwa makini na waadilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi linatorajiwa kufanyika mnamo tarehe 23 mwezi wa nane ,2022.
Mhe Masala, ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo kwa washiriki 1346 ambayo yaliyotolewa kwa takribani siku 19 huku akiwakumbusha juu ya kuzingatia wajibu wa kazi iliyowapeleka ikiwa ni pamoja na kuepuka upikaji wa taarifa.
“Tunaamini katika mafunzo mliyopatiwa mmeelezwa uadilifu na umakini na kazi zetu nenda kachukue dodoso ya kile kilichokupeleka ukimaliza ondoka usiende kufanya yaliyo nje na hayo na msije kusahau wajibu wa kazi iliyowapeleka”, amesema Mhe Masala.
Pamoja na hayo amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutambua thamani ya kazi wanayoenda kufanya kwani dhamana waliyopewa ni kubwa na kusisitizwa kutokutanguliza mbele maslahi bali kuangalia ni nini wamelifanyia Taifa la Tanzania kwani chochote watakacholipwa hakina thamani kwa kazi kubwa iliyopo mbele yao
“Zoezi hili serikali imewekeza muda, rasilimali fedha , vifaa vyenye thamani kubwa kwa kufanya hayo yote hata wewe uliyepewa dhamana ya kufanya kazi hii lazima utambue thamani ya kazi ambayo unayoenda kufanya usiangalie unalipwa nini angalia umeisaidia taifa lako kwa kiasi gani kufanikisha zoezi hili hiyo ndio sifa kubwa utakayoondoka
Nae mratibu wa Sensa ya watu na makazi 2022 Wilaya ya Ilemela , Ndugu Yohanne Magesa ametoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kufanya kazi kwa vitendo, hiari na kwa moyo na kuwahimiza kuangalia uzalendo wa Taifa la Tanzania.
Ndugu Said Kitinga ambae ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela amewapongeza washiriki hao kwa kupata nafasi ya kuweza kushiriki zoezi la kitaifa la sensa na kuwataka kujiona kuwa wao ni wa thamani kwani wamepata nafasi ya kipekee ambapo aliwasisitiza kufanya kazi hii kwa ueledi na pia kwenda kuitumia elimu waliyopewa mara baada ya zoezi la sensa kukamilika.
Nao washiriki wa mafunzo hayo ya sensa ya watu na makazi wamemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa nasaha zake na kuzitaja changamoto zilizojitokeza wakati wakifanya mazoezi kwa vitendo likiwemo suala la baadhi ya wananchi kuonyesha kutokuwa tayari kushiriki zoezi hilo hivyo kuomba elimu zaidi kutolewa katika siku zilizobakia.
Zoezi hili la kufunga mafunzo ya Sensa ya Watu na Makazi limeambatana na zoezi la uapishwaji ambapo washiriki wote waliapishwa kiapo cha utii, uadilifu na uaminifu mbele ya Waheshimiwa mahakimu Leonard. H. Ndolezi na Cindy Kaaya na kukumbushwa kuwa kiapo kimetolewa kwa mujibu wa sheria ya Takwimu ya Sura Na 351, sheria inayosimamia masuala ya Sensa nchini huku wakionywa kutunza siri zote.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.