UKAMILISHWAJI WA UJENZI WA JENGO LA DHARULA LA HOSPITALI YA WILAYA WALENGA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA ILEMELA
Vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinatarajiwa kupungua ndani ya manispaa ya Ilemela baada ya kukamilika kwa jengo la kisasa la dharula la hospitali ya wilaya hiyo likijumuisha kamera za usalama na mifumo yote ya kisasa ili kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanapata huduma bora na salama za afya
Hayo yamebainishwa na mchumi wa manispaa hiyo ndugu Amosi Zephania wakati akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo jipya la dharula na inayotegemewa kuwa hospitali ya wilaya kwa kamati ya fedha ya manispaa ilipotembelea eneo hilo kuona namna shughuli za ujenzi zinavyoendelea
‘… Manufaa ya mradi huu utakapokamilika ni kupunguza vifo vya wakina mama wajawazito na watoto wachanga, kupunguza msongamano wa wagonjwa hasa katika hospitali ya rufaa ile ya mkoa Sekou Toure na kupunguza usumbufu kwa jamii kufuata huduma kwa umbali mrefu …’
Aidha ameongeza kuwa mbali na jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kufanikisha ujenzi huo bado ipo changamoto ya kifedha na kuomba serikali kuu kusaidia ujenzi huo
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya fedha ambae pia ni mstahiki meya wa manispaa mheshimiwa Renatus Mulunga amesema kuwa ameridhishwa na namna ujenzi unavyoendelea na kuongeza kuwa mbali na msaada wa serikali kuu manispaa yake itayatumia mapato yake ya ndani kusaidia kukamilika kwa ujenzi huo kila panapowezekana
‘… Naridhishwa na hatua za ujenzi, Ni hatua nzuri kazi iendelee zaidi pesa tu iongezwe ili tukamilishe ujenzi huu kwa haraka …’ alihitimisha
Ujenzi wa jengo la kisasa la dharula mpaka sasa umegharimu zaidi ya shilingi milioni mia tano na tatu na mpaka kukamilika kwake inategemewa kugharimu zaidi ya shilingi milioni mia sita tisini na nne ambapo mpaka kukamilika kwa hospitali yote ya wilaya inategemewa kugharimu zaidi ya bilioni Ishirini na tano na umechukua eneo la ukubwa wa zaidi ya heka mbili na nusu
Mbali na hayo Kamati pia ilifanikiwa kuzuru mradi wa usambazaji maji Kahama-Nyamadoke na baadae kuzungumza na wafanya biashara wa soko la mbao Sabasaba ikiwa ni jitihada za kuhakikisha inawasaidia wafanya biashara wa masoko yake sambamba kuongeza mapato ya serikali.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.