Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ilemela inayojengwa katika eneo la Isanzu kata ya Bugogwa hadi leo tarehe 12/07/2019 umefikia takribani asilimia 85 ya utekelezaji wa mradi ambapo majengo yote saba yamekamilika na shughuli zinazoendelea kwa sasa ni ukamilishaji kwa maana ya kuweka vigae, kupaka rangi, kuweka vioo vya aluminium, uwekaji wa gata za maji, mfumo wa maji taka pamoja na kusafisha maeneo ambapo ujenzi unaendelea.
Jumla ya Majengo saba ya awali yanayojengwa ni pamoja na;Jengo la utawala, Jengo la wagonjwa wa nje (OPD), Stoo ya dawa, Maabara, Jengo la vipimo vya Mionzi, Jengo la kufulia nguo (Laundry) pamoja na Jengo la Wazazi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela John Paul Wanga akiongelea kuhusu ujenzi huu amesema kuwa, Ujenzi wa hospitali ya Wilaya ulianza mnamo tarehe 22/3/2019 na unajengwa kwa kutumia force account chini ya usimamizi wa kamati 5 zilizoundwa ambazo ni kamati ya ufuatiliaji na utawala, kamati ya ununuzi, kamati ya mapokezi, kamati ya utunzaji na ufuatiliaji wa vifaa pamoja na kamati ya ujenzi ambapo kila kamati ina mwakilishi kutoka kwenye jamii.
Aidha aliongeza kuwa hospitali hiyo itakapokamilika inatarajia kuhudumia wakazi 457,774 wa Ilemela pamoja na maeneo jirani huku akimshukuru Mhe Rais kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya.
“Kwa niaba ya wananchi wa Manispaa ya Ilemela, nimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kutupatia fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huu kwani Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela haikuwa na hospitali ya wilaya na wananchi wake walitegemea kuhudumiwa na hospitali ya rufaa ya mkoa, hospitali ya jeshi pamoja na hospitali ya kanisa la wasabato”, alisema Mkurugenzi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni kati ya halmashauri 67 nchini zilizopatiwa fedha kiasi cha Tsh. Bil 1.5 toka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya katika mwaka wa fedha 2018/2019, ambapo fedha hiyo ililenga kutumika kwa ajili ya ujenzi wa majengo 7 ya awali yaliyokamilika kwa asilimia 100 kati ya majengo 22 ambayo yanatakiwa kujengwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.