Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa uchumi wa bluu ni fursa kubwa na yenye kuwezekana kutokana na uhitaji mkubwa wa mazao ya samaki nchini na nje ya nchi.
Ameyasema hayo alipotembelea mradi wa vijana wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba uliopo Kata ya Sangabuye eneo la Igalagala ambapo amewapongeza vijana hao kwa hatua hiyo waliyofikia na kuwataka waombe mkopo ili waweze kuwa na vizimba hata 30 kuwawezesha kupata samaki wengi zaidi, pesa nyingi zaidi ili waweze kuajiri na vijana wengine. Kwani kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara takriban vizimba 600 vinawezekana kuwekwa katika eneo la ziwa Viktoria.
“Ninaamini uchumi wa bluu ni fursa kubwa na yenye kuwezekana, kwa mujibu wa takwimu nchi ya ubelgiji na ufaransa wanataka tani 10 za samaki aina ya dagaa kila mwezi kutoka katika nchi yetu hivyo hatuna sababu ya vijana kukosa ajira endapo tuta jipanga vizuri na tukawajibika kila mmoja akapambana kwa dhati kabisa”, amesema Mhe Ulega
Aidha amesema kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameweka fedha jumla ya Tsh. Bilioni 20 katika benki ya kilimo kwa ajili ya kuweza kuinua makundi ya vijana, wakinamama na watanzania wote wenye kutaka kufanya kazi ya uzalishaji mali ili kulijenga taifa la Tanzania kupitia fursa ya uchumi wa bluu. Huku akiwasisitiza vijana ambao tayari wameianza hii kazi na wanaotarajiwa kuanza na walio na utayari, fedha hizi zipo tayari ziingie katika uzalishaji.
Pamoja na hayo ameupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kwa uthubutu na kuweza kutoa takriban milioni 90 na kuzipeleka katika sekta ya uzalishaji ili kuweza kuwainua vijana hawa wa kitanzania.
“Hii Manispaa imekuwa ya mfano katika jambo hili la kuwezesha vijana katika suala la ufugaji samaki kwa njia ya vizimba na mimi nitakuwa balozi wenu na shahidi kadiri nitakavyopata nafasi ya kusema kwamba mfano mzuri umeonyeshwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela”. Amesema Mhe Ulega
Mhe. Hasan Masala, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amesema kuwa uongozi wa Ilemela unaendelea kuvisimamia vikundi hivyo ili viweze kutimiza malengo na kuwa vya mfano , pamoja na kuendelea kuvifuatilia ili viweze kupewa fedha nyingi zaidi na kuleta mapinduzi ya uchumi wa blue kupitia vikundi vya vijana wanawake na walemavu.
Vikundi hivyo vya Catfish na chapakazi ambavyo vilipata mkopo wao kupitia Halmashauri kiasi cha Shilingi milioni 91 za kitanzania kwa ajili ya kuanzisha mradi vinatarajia kuvuna tani 16 ya samaki yenye thamani ya Tsh Milioni themanini za Kitanzania kutoka katika kila kizimba kimoja cha samaki, amesema ndugu Baraka ambae ni kiongozi wa kikundi cha catfish
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.