Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe. Renatus Mulunga amewataka waheshimiwa madiwani na watalaam kukusanya mapato kwa kiwango kikubwa ili kuweza kuitekeleza bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Ametoa rai hiyo wakati wa kikao cha baraza la madiwani ambalo liliketi kwa ajili ya kupitia mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo amesema kuwa, suala la kupitisha bajeti ni suala moja lakini bajeti haiwezi kutekelezeka kama tulivyoipitisha kama wote kwa pamoja hatutashirikiana katika suala zima la ukusanyaji wa mapato
“Nitoe rai kwa wakazi wote wa manispaa ya Ilemela kupitia kata zetu kuhakikisha wanalipa tozo zote kama inavyowapasa pamoja na hilo niwatake waheshimiwa madiwani tuwe pamoja katika suala la ukusanyaji wa mapato kwan tukikusanya vyakutosha haya tuliyoyapitisha yataweza kutekelezeka na kama hatutakusanya tutaendelea kupitisha na utekelezaji hautafanyika” amesema Mhe Mulunga
Wakichangia bajeti hiyo kwa nyakati tofauti madiwani wamepongeza kwa namna ambavyo bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuwa imeangalia sekta mbalimbali ikiwemo suala la ukamilishaji wa miradi viporo huku wakihimiza suala la utekelezaji wa bajeti ili wote kwa pamoja tuwe mfano na kusisitiza kuwa wataalam wasimamie kwa makini ili bajeti ilete tija
Akichangia kuhusu mikopo ya asilimia 10, diwani wa viti maalum Mhe Sarah Lisso amepongeza kwa halmashauri kuwakopesha vijana na kuweza kuanzisha mradi mkubwa wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba huku akishauri jambo kama hilo lifanyike pia kwa vikundi vya wanawake badala ya kupewa fedha wasimamiwe kuanzisha mradi ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Mhe Maganiko kutoka kata ya Nyamanoro akichangia bajeti hiyo ameomba bajeti hiyo iangalie suala la utunzaji wa maeneo ya makaburi kwa ajili ya kuwasitiri ndugu waliotangulia pamoja na kushauri juu ya suala la ununuzi wa greda kwa ajili ya kuboresha barabara katika kata mbalimbali za Halmashauri kwani malalamiko ni wengi kwa wananchi yanayohusiana na ubovu wa barabara.
Mhandisi Modest Apolinary, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, amefafanua masuala mbalimbali kuhusiana na bajeti na kusema kuwa hii ni rasimu ya bajeti hivyo amepokea maoni yote na kuahidi kuyafanyia kazi kabla ya kuwasilishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya kusomwa katika bunge la bajeti.
Awali akiwasilisha bajeti hiyo Mchumi wa Manispaa Ndugu Herbert Bilia amesema Halmashauri imekadiria kukusanya na kutumia jumla ya Shilingi Bilioni 71.57 ambapo kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 8.39 ni kwa ajili ya Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo, Shilingi bilioni 45.29 ni Mishahara, Shilingi bilioni 1.65, Ruzuku ya Matumizi ya Kawaida.
Kwa upande wa mapato ya ndani Ndugu Bilia amesema kuwa Halmashauri inakisia kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 16. 23 ambapo Shilingi bilioni 8.76 kati ya fedha hizo za mapato ya ndani ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na shilingi bilioni Tshs 5.84 ni matumizi ya kawaida na Shilingi Bilioni 1.61 ni mapato fungwa.
Bajeti hii ya mwaka wa fedha 2023/2024 imepanda kutoka Shilingi Bilioni 67.77 ya mwaka 2022/2023 hadi kufikia Shilingi bilioni 71.57 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 5.6. Amesema ndugu Bilia.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.