“Tuwe na uvumilivu serikali inatafakari njia bora ya kutatua mgogoro huu ambao umedumu kwa muda mrefu, lengo la kufika hapa leo ni kuwahakikishia wananchi kuwa serikali haina haja ya kumdhulumu mwananchi yoyote na pia inawajali na kuwathamini”. RC Mtanda
Mhe Said Mtanda, Mkuu wa mkoa wa Mwanza ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya Shibula siku ya tarehe 21/02/205 kufuatia mgogoro wa ardhi unaoendelea kati ya wananchi na eneo la uwanja wa ndege wa Mwanza.
Mhe Mtanda aliendelea kusema kwa kuwataka wananchi kuendelea kuwa na Subira, amani na utulivu wakati serikali inatafakari namna bora ya kutatua mgogoro huu huku akiwahakikishia kuwa serikali hii ni sikivu.
“Tunafahamu kuwa ni muda mrefu sasa mmezuiliwa kuendeleza maeneo yenu kutokana na mgogoro huu, lakini mimi kama kiongozi siwezi kuwapa majibu mepesi kwa lengo la kuwaridhisha, niwahakikishie kuwa maoni yenu yamepokelewa na yanafanyiwa kazi”. RC Mtanda
Akiwasilisha mapendekezo kwa niaba ya kamati ya kata iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo, ndugu Deus Kaji alisema kuwa kamati inaiomba serikali kuhakikisha kuwa inaumaliza mgogoro huo ili waweze kuendelea na maisha kama wananchi wengine wakipendekeza ifuatavyo;Kulipwa fidia ya maeneo yao, serikali iwaachee waendeleze maeneo yao, kupewa maeneo mbadala ili wapishe eneo hilo sambamba na mapendekezo hayo wameomba wapewe fomu namba moja ya utambuzi wa mali na thamani halisi ya maeneo yao.
Mgogoro huo wa ardhi wa mpaka uwanja wa ndege na wananchi wa kata ya Shibula uliodumu zaidi ya miaka 8 unawahusu wananchi takriban 5471 kutoka katika kaya zaidi ya 1404 za mitaa mitano ambayo ni Nyamwilolelwa, Kihiri, Shibula, Mhonze B na Bulyangh’ulu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.