Afisa tarafa wa Wilaya ya Ilemela ndugu Godfrey Mnzava kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela ameshiriki maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika katika viwanja vya zahanati ya Nyerere iliyopo kata ya Buswelu.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za UKIMWI katika Wilaya ya Ilemela wakati wa maadhimisho hayo Tabibu huduma ya tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya vya UKIMWI zahanati ya Nyerere Phidon Byangwamu amesema hali ya maambukizi ya VVU imeshuka kutoka 5% mwaka 2022 hadi kufikia 3.4% mwaka 2023.
Akipokea taarifa hiyo Mnzava amepongeza juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali na wahudumu wa afya katika mapambano dhidi ya UKIMWI huku akiwataka wazazi na walezi kutoona aibu kuzungumza na watoto masuala ya elimu ya uzazi na UKIMWI.
" Tulipofika hakuna kuoneana aibu tena ndani ya familia tuwafanye watoto kuwa marafiki zetu wawe huru kusema chochote kinachowatatiza na tuzungumze nao kwa undani masuala ya makuzi na UKIMWI ."
Aidha ameitaka jamii kuunga mkono kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo "jamii iongoze kutokomeza UKIMWI" kwa kujihadhari na tabia ambazo zinaweza kupelekea kupata maambukizi mapya kama vile ngono zembe na kuchangia matumizi ya vitu vyenye ncha kali wakati wa tohara na kuiasa jamii kujitokeza kupima afya ili kujua afya zao na kupata ushauri wa kitaalam kwa hali zote.
Robert Ngaiza ni mkazi wa Buswelu yeye anawasihi wanaume wenzie kujitokeza kwa wingi kupima UKIMWI kwani takwimu zinaonyesha wanaopima kwa wingi ni wanawake.
" Jamani tujitokeze kupima mambo ya kumsubiri mama akiwa mjamzito akienda kliniki apime akuletee majibu sio sawa,yale ni majibu yake yeye sio yako.Tusiogope kwani hata alieambukizwa bado ana nafasi ya kufanya vitu vingi vya kimaendeleo na kutimiza ndoto zake ikiwa utafuata ushauri wa wataalam wa afya."
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.