Mwandishi: Afisa Habari Ilemela
Ualimu ni miongoni mwa kada kongwe duniani ni fani inayombadilishia mtu muelekeo kutoka muelekeo mbaya kuelekea ulio sahihi. Kazi ya mwalimu inajumuisha mambo mengi sambamba na vita vya kupambana na ujinga. Hivyo yatupasa tumpe heshima kubwa na ya pekee kwa vita kubwa anayopambana nayo katika jamii yetu ya kupambana na adui ujinga.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ambae alikuwa mgeni rasmi katika sherehe ya kuwapongeza walimu wote wa shule za msingi Ilemela kwa matokeo mazuri ya wastani wa A kwa miaka mitatu mfululizo.
“Wewe na mimi tusingekuwa hapa tulipofika bila mchango wa mwalimu, majukumu ya mwalimu ni kubadilisha fikra kuondoa kitu kigeni kuweka kitu kipya, kuondoa kitu kisicho sahihi kuweka kilicho sahihi kumbadilishia mtu mwelekeo anapotaka kuingia kwenye shimo huambiwa hapa sio sahihi njia ya kupita ni hii, sio jambo dogo walimu wanastahili pongezi na heshima kwenye jamii”, alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mkuu wa Mkoa, alitumia fursa hiyo pia kuwatia moyo walimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi na kuwaeleza kuwa uongozi wa mkoa unatambua changamoto zao huku akizitaka halmashauri zote ndani ya mkoa wa Mwanza kuweka mikakati ya kuzitatua changamoto zao ili kuwawezesha walimu kuwajibika kwa viwango vya juu katika maeneo yao ya kazi.
“Tunapohitaji mabadiliko ya wanafunzi, tunapohitaji kupata matokeo ya bidhaa yoyote ile angalia mtambo unaohusika na uzalishaji wa bidhaa.Huwezi kujenga jamii yenye nguvu kama jeshi unalotumia ni jeshi lililokata tamaa hivyo tuwatie moyo walimu kwenye changamoto zao ambazo nyingi ziko kwenye uwezo wetu, kwa kuondoa changamoto za nyumba za walimu, vyumba vya madarasa pamoja na ofisi za walimu.Kwa hiyo ni lazima tuweke uwekezaji mkubwa katika kumlinda mwalimu na vita hii niko tayari kupigana na ilemela”,Alisema Mhandisi Gabriel
Mhe Hasan Masala Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuitikia wito wa kuwa mgeni rasmi, na kumuahidi kuwa kwa mwaka 2022 na miaka ijayo Ilemela itashika nafasi ya kwanza kitaifa na kimkoa kwani sababu za kuwa wa kwanza zipo na walimu wameshakula kiapo na kuahidi kuwa wanaenda kushika nafasi ya kwanza chini ya usimamizi wa viongozi wa Wilaya.
Akiwasilisha salam za Chama cha walimu Wilaya ya Ilemela, Zephania Sabuni, ambae ni katibu wa Wilaya Ilemela, alisema kuwa hii ndio hamasa inayohitajika kwa ajili ya kupata maendeleo ya elimu yaliyotukuka aliongeza kusema kuwa ni muhimu suala hili kuendelezwa kwani ni moja ya vitu vinavyowatia moyo na nguvu waalimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Mwalimu Dismas Hamaro ambae ni mwalimu mkuu katika shule ya msingi ya Mnarani, kwa niaba ya walimu wote, amezitaja mbinu watakazoendelea kuzitumia katika kuboresha ufaulu zaidi ikiwa ni pamoja na kuendelea na maboresho ya elimu ya KKK, kutoa elimu ya kujitambua na uzazi kwa wanafunzi na kuendelea kuhamasisha jamii kuendelea kuchangia juhudi mbalimbali za kimaendeleo.
Pamoja na hayo wametoa shukran kwa uongozi wa halmashauri kwa jitihada za ujenzi wa miundombinu inayopelekea kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, ofisi za walimu matundu ya vyoo nyumba za walimu na utenegenezaji wa madawati kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri huku wakiahidi kuendelea kutenda kazi kwa bidii na maarifa.
Nae Mwalimu Richard Jeremiah wa shule ya msingi Nyamhongolo alisema kuwa uongozi wa Ilemela umefanya vyema kuwakutanisha na kuwapongeza walimu kwa kufaulisha.
“Ni jambo jema kwa viongozi na wakuu wetu katika kazi kutambua jitahada zetu kwa namna hii,mtu anapopongezwa kwa maneno na zawadi anahamasika zaidi kufanya vizuri.Namuunga mkono Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kwamba tunaweza kuwa wa kwanza kitaifa kwani kwa hili lililotokea hapa leo najisikia vizuri sana na nipo tayari kwa kazi, Naipenda kazi yangu ya ualimu.” Alisema Mwl.Richard.
Mwalimu Jamila khalfan Afisa taaluma wa shule za msingi katika Manispaa ya Ilemela alisema kuwa, kupitia viongozi wetu wameendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ,huku akiwaasa walimu kufanya kazi kwani mtaji wa mwalimu ni taaluma hakuna atakaesifika nje ya taaluma, kwani taaluma inapopanda ndipo unaposifika.
Katika hafla hiyo ya kuwapongeza walimu, iliyotangulia na mashindano ya michezo mbalimbali, uongozi wa Manispaa ya Ilemela,ulitoa zawadi mbalimbali pamoja na vyeti kwa walimu bora wa masomo kwa mwaka 2021, shule 10 bora kwa mwaka 2021 pamoja na zawadi za jumla kwa shule zote za Msingi. Zawadi zilizotolewa ni pamoja mifuko ya sukari ya ujazo kilo 25, pamoja na televisheni ya ukubwa inchi 32 ikiwa ni nyenzo ya kufundishia kwa sule 10 bora kwa mwaka 2021.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.