Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela ndugu Marco Busungu amesema Ilemela inaendelea kuunga mkono jitihada za Mhe.Rais katika kutunza mazingira kwa kupanda miti mingi zaidi katika kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha mkoani Mwanza ambapo Ilemela ni moja ya wilaya ndani mkoa huu.
Akizungumza wakati akipokea miti 5,000 kutoka wakala wa misitu (TFS)-Mwanza, Busungu amesema ni jukumu la jamii nzima kutunza miti kwa kuzingatia faida zake nyingi katika maisha ya binadamu.
"Ilemela tunaendelea kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais Mhe.Mipango anayoendelea kuyatoa maeneo mbalimbali katika ziara zake juu ya utunzaji wa mazingira sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika masuala mazima ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi." Amesema Busungu
Alex Julias ni mhifadhi misitu na nyuki kutoka TFS -MWANZA anasema kampeni ya upandaji miti imeanzia shule za msingi kwa sababu ni sehemu inayomjenga mtoto kuwa na mazoea ya kufanya jambo mara kwa mara bila kusahau hivyo watoto wakielekezwa vizuri ni mabalozi wa kudumu katika suala la utunzaji wa mazingira.
Afisa elimu mazingira ndugu Beatus Kahulu amewashukuru TFS -MWANZA kwa wepesi wao wa kuitika wito na kujibu ombi la Ilemela kwa kutoa miche hiyo huku akiwataka walimu, wanafunzi na wazazi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ili ilete tija ilokusudiwa.
Nae Anthony Goodlucky mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Kiseke amezitaja baadhi ya faida za upandaji miti ikiwa pamoja na miti kuzalisha hewa safi ya oksijeni,baadhi ya miti ni chanzo cha mapato mfano miti ya mbao,miti ya matunda ni faida katika masuala ya lishe bora na pia miti hutoa vivuli hasa nyakati za jua.
Jumla ya miche ya miti 5,000 iliyopokelewa kutoka TFS imejumuisha miti ya mbao,kuni,nguzo na matunda kama parachichi .
MWISHO
Imetolewa na;
Kitengo cha mawasiliano serikalini -Manispaa ya Ilemela
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.