Tathimini za utendaji kazi na mabadilishano ya uzoefu na changamoto yatasaidia uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya ndani ya wilaya ya Ilemela
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za uchumi afya na elimu ya Manispaa ya Ilemela ambae pia ni Diwani wa kata ya Ibungilo Mhe Husein Magera wakati wa kikao kazi cha tathimini cha viashiria mbalimbali katika huduma za afya zinazotolewa na vitengo vinavyopatikana katika divisheni ya afya, huduma na lishe ambapo amewapongeza watoa huduma za afya manispaa ya Ilemela pamoja na kuwataka kutovunjika moyo katika kutoa huduma bora Kwa wananchi
'.. Niwapongeze maana tathimini ya utendaji kazi wetu inatupa picha ya namna bora ya kufanya, kupitia tathimini tunabadilishana mawazo, itatusaidia namna ya kubadilishana changamoto tulizonazo, Changamoto za Sangabuye haziwezi kuwa sawa na za Buzuruga ..'
Aidha Mhe Magera amewashukuru wataalam wa sekta ya afya na kusisitiza kuwa wanafanya kazi kubwa na kwamba wanapaswa kutiwa moyo
Halikadhalika Mganga mkuu wa Manispaa ya Ilemela Daktari Marwa Samson amefafanua kuwa lengo la kikao hicho cha tathmini ni kupata uhalisia wa taarifa za utoaji huduma zinazotolewa na vituo vya afya na zahanati katika mitaa na kata walipo wananchi
Nae Katibu wa afya manispaa ya Ilemela Bi Emila Msengi amesema kuwa ipo haja ya kushawishi na kufanya zoezi la utoaji wa elimu ya afya kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya Kamati za maendeleo za ngazi za mitaa na kata (WDC)
Nyabwire Lukumay ni mratibu wa huduma za mama na mtoto manispaa ya Ilemela ametaja visababishi vya vifo vya wazazi katika taarifa yake ya kuanzia Januari hadi Novemba kuwa ni wajawazito kutopata matibabu sahihi kipindi cha ujauzito, ufuatiliaji hafifu wa wajawazito wanaogundulika na vidokezo hatari pamoja na kutowafuatilia wakina mama wenye uchungu pingamizi
Leah Matondo ni mganga katika zahanati ya Nyerere kata ya Buswelu, yeye amepongeza kufanyika kwa kikao hicho cha tathimini za huduma za afya na kwamba kupitia kikao hicho ameweza kupata uzoefu mpya sanjari na kushauri utaratibu huo uwe endelevu Ili wataalam wa sekta ya afya waweze kupata uzoefu mpya na kubadilishana changamoto wanazokutana nazo katika kuhudumia wananchi
Tathimini hii kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2023 imelenga kuboresha na kupima utendaji kazi kwa waliofanya vizuri na waliofanya vibaya ili kuweza kuweka mpango kazi wa mikakati kwa ajili ya maboresho katika maeneo ambayo walifanya vibaya. Sambamba na kujadili vifo vya wamama wajawazito na watoto wachanga ili kuweza kufahamu sababu zilizopelekea vifo na kutengeneza mpango kazi wa kuboresha ili kuepukana na vifo hivyo
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.